MSEMAJI MKUU WA SERIKALI AONYA USAMBAZAJI HABARI ZA UONGO, PICHA ZISIZO NA STAHA AJALI YA MOTO MOROGORO


Na Betrice Lyimo - MAELEZO
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, ametoa onyo kwa wananchi kuacha kusambaza picha za miili ya wananchi walioathirika na moto uliotokana na mlipuko wa mafuta yaliyokuwa kwenye lori lililopinduka asubuhi ya leo mkoani Morogoro.

Dkt. Abbasi amesema: “Ni kinyume cha sheria na utamaduni wa Mtanzania kusambaza picha za watu wakiwa kwenye hali ya fadhaha”.

Dkt. Abbasi ametoa kauli hiyo leo mchana Agosti 10, 2019 katika mahojiano maalum kupitia Televisheni ya Taifa (TBC) kuhusiana na ajali hiyo.

Katika mahojiano hayo, Msemaji Mkuu wa Serikali amewaasa wananchi kuacha kusambaza habari zisizokuwa na uhakika ili kuepusha upotoshaji wa taarifa.

"Niwaombe wananchi kuacha kusambaza habari za uongo kuhusu idadi ya vifo na majeruhi wa ajali. Ni muhimu sana watumie vyanzo rasmi vya Serikali kupata taarifa hizo ambavyo kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro (RPC) Wibrod Mtafungwa” ameeleza Dkt. Abbasi.

Aidha Dkt. Abbasi ameviasa vyombo vya habari kufuata maadili ya uandishi wa habari kwa kuandika habari sahihi na kupiga na kutumia picha zilizo na staha ili kuepusha taharuki katika jamii.

Ajali hiyo imetokea leo tarehe 10 Agosti, eneo la Msamvu mkoani Morogoro ambapo Lori lililokuwa limebeba shehena ya mafuta lilipinduka na baade kulipuka moto.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527