MSD KUFUNGUA KITUO CHA UUZAJI NA USAMBAZAJI DAWA SIMIYU

Na Stella Kalinga, Simiyu RS

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya dawa (MSD)  Laurean Bwanakunu amesema Bohari ya dawa inatarajia kuanza ujenzi wa kituo cha mauzo na  usambazaji  dawa mkoani Simiyu ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa mkoa wa Simiyu na mikoa jirani.

Bwanakunu ameyasema hayo Agosti 19,2019 katika ufunguzi wa  mkutano wa tathmini ya utendaji  kazi wa menejimenti na mameneja wa kanda wa bohari ya dawa nchini.

Lengo likiwa   ni kujenga ushirikiano na kufanya kazi kwa timu.

Bwanakunu amesema wameamua kufanyia mkutano wa tathimini mkoani Simiyu ili kuweza kujionea eneo la ujenzi wa kituo cha mauzo ya dawa ikiwa ni moja ya kuongeza wigo mpana wa utoaji huduma.

“Tutakuwa na mkutano wa siku tatu hapa Simiyu kwa ajili kufanya tathmini ya utendaji kazi ulivyokuwa kwa mwaka mzima, tutawafanyia tathmini wakurugenzi wote na wenyewe watamfanyia Mkurugenzi Mkuu; lakini pia tutatumia fursa hii kutembelea mahali tulipoamua kujenga bohari kwa kuwa tunatarajia kujenga bohari hapa Simiyu”alisema Bwanakunu.

Akifungua mkutano huu, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema  maboresho ya usambazaji wa dawa yaliyofanywa na Bohari ya Dawa (MSD) yameongeza upatikanaji wa dawa mkoani Simiyu ambapo kwa sasa upatikananji wa dawa ni zaidi ya asilimi 88.

Aidha, Sagini ametoa wito kwa Taasisi zote za Umma zinazohitaji maeneo kwa ajili ya kujenga Ofisi zao kufika mkoani Simiyu, ambapo amewahakikishia upatikanaji wa maeneo lengo likiwa ni kuendelea kusogeza huduma mbalimbali karibu na wananchi.

Mkurugenzi wa Rasilimali watu wa  Bohari ya Dawa(MSD), Bibi. Victoria Elangwa amesema uwepo wa kituo cha kusambaza dawa Simiyu kutapunguza umbali kwa Mkoa wa Simiyu na mikoa ya Mara na Shinyanga  kupata huduma za Bohari ambazo kwa sasa zinapatikana Mwanza.

Ameongeza kuwa ujenzi wa Kituo hicho unatarajia kuanza mara moja kwa kuwa tayari wataalam wameshaanza kushughulikia masuala ya ukamilifu wa mazingira na baada kukamilisha kazi hiyo atatafutwa mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527