MFANYAKAZI TAKUKURU MAKAO MAKUU ADAKWA AKIOMBA NA KUPOKEA RUSHWA


Mchunguzi Mkuu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (Takukuru), Cosmas Batanyita (44), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Tanzania  akikabiliwa na mashtaka saba likiwemo la kuomba rushwa ya Sh200 milioni na kutakatisha fedha.

Batanyita ambaye ni mkazi wa Chamazi, Dar es Salaam amefikishwa mahakamani hapo, leo Ijumaa Agosti 9, 2019 na kusomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina.

Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiana kusomewa mashtaka yake na Wankyo Simon amedai mshtakiwa huyo anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 76/2019.

Miongoni mwa mashtaka yanayomkabili mshtakiwa huyo ni kushawishi, kuomba rushwa na kutakatisha fedha, ambapo anadaiwa kuyatenda kati ya Februari  9, 12 na 24, 2019.

Katika shtaka la kuomba rushwa, Batanyita anadaiwa Februari 9, 2019 eneo la Upanga, Dar es Salaam akiwa mwajiriwa wa Takukuru alishawishi na kuomba rushwa ya Sh200 milioni kutoka kwa Hussein Gulamal Hasham ili aweze kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji wa kodi iliyokuwa inamkabili Hasham.

Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili, hakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana.

Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 23, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa  rumande.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post