MSAFARA WA MKUU WA WILAYA WAPIGWA MAWE

Picha haihusiani na habari hapa chini

Na Hawa Mathias, Mwananchi 
Msafara wa wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Kyela umezuiwa na kundi la vijana waliovalia mashati mekundu.

Vijana hao walipanga mawe na magogo barabarani na kusababisha magari ya viongozi wa kamati hiyo kusimama. Miongoni mwa waliokuwepo katika msafara huo ni mkuu wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kitta.

Akizungumza leo Alhamisi 29, 2019 mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Hunter Mwakifuna amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akibainisha kuwa ilikuwa jana Jumatano Agosti 28, 2019 saa 11 jioni katika kijiji cha Mpuguti kata ya Makwale.

Amesema walikuwa wakitoka kukagua miradi itakayotembelewa na mbio za mwenge wa uhuru wilayani humo Jumatatu Septemba 9, 2019.

Amebainisha kuwa katika tukio hilo watu wawili wamejeruhiwa kwa mawe akiwepo ofisa usalama wa wilaya hiyo na katibu wake.

“Tunashukuru Mungu vyombo vyetu vya usalama vilikuwa makini katika mapambano, gari ya mkuu wa wilaya iligeuzwa na kurudi ilipotoka,” amesema.

Amebainisha kuwa mpaka sasa watu 45 wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na tukio hilo, bado uchunguzi unaendelea.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post