KIJANA ATUPWA JELA MIAKA 60 KWA KUMBAKA NA KUMPA MIMBA MWANAFUNZI KAHAMA

Na Salvatory Ntandu -Malunde1 blog Kahama
Mkazi wa kijiji cha Izumba kata ya Ikinda katika halmashauri ya Msalala wilayani kahama mkoani Shinyanga Maneno Hungwi (19) amehukumiwa kifungo cha miaka 60 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi mwenye umri wa miaka 17.

Hukumu hiyo imetolewa Agosti 28,2019 na Hakimu mkazi wa Mahakama ya wilaya ya Kahama Ushindi Swalo na kusema kuwa Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ambao umethibitisha kuwa Maneno alitenda kosa hilo.

Amesema Mahakama imepitia hoja zote zilizowasilishwa na pande zote katika shauri hilo na kijiridhisha pasipo shaka yeyote kuwa Maneno alitenda kosa hilo Aprili tano mwaka 2018 na anastahili adhabu hiyo.

Hakimu Ushindi amesema Maneno atatumika adhabu hiyo ili iwefundisho kwake na kwa watu wengine kwenye jamii wanaotenda jinai hizo kwa makusudi kwa wanafunzi huku wakijua wazi kuwa ni kosa.

Kabla ya kutolewa hukumu Maneno aliomba Mahakama impunguzie adhabu kwani ni kosa lake la kwanza hoja ambayo imetupiliwa mbali na Mahakama hiyo.

Awali mwendesha mashitaka wa Jeshi la Polisi Inspekta Peter Masau wakati akisoma shauri hilo la jinai namba 268 la mwaka 2018 amedai mahakamani hapo kuwa, Maneno alitenda kosa la kubaka kinyume na kifungu 130 (1)(2)(e) na131(1) sura ya 16 ya kanuni ya adhabu marejeo ya mwaka 2002.

Katika kosa la pili Maneno anadaiwa kumpa mimba mwanafunzi kinyume na fungu 60 A sura ya 353 ya sheria ya elimu ya mwaka 2016.

Tayari Maneno ameanza kutumikia hukumu yake na Mahakama imetoa haki ya kukata rufaa ndani ya siku 60.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527