KILICHOENDELEA LEO MAHAKAMANI KATIKA KESI YA FREEMAN MBOWE NA VIGOGO WENGINE WA CHADEMA


Shahidi wa sita wa upande wa Jamuhuri katika kesi ya tuhuma za uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwemo Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, ameieleza Mahakama video iliyoangaliwa mahakamani kama sehemu ya ushahidi wake, hakukuwa na mahali ambapo panaonesha askari polisi wakishambuliwa na wafuasi wa chama hicho.

Pia amedai katika mkutano huo wa kumnadi aliyekuwa mgombea wa ubunge wa Jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam Salum Mwalimu hakukuwa na wafuasi wa Chadema waliokuwa wanahutubiwa ambao walikuwa wameshika silaha.

Shahidi huyo Koplo Charles amedai hayo leo Agosti 20,mwaka 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alipokuwa akijibu maswali ya Wakili wa utetezi Peter Kibatala.

Amedai katika ushahidi wake huo wa video ambao mahakamani hapo umepokelewa kama kielelezo namba tano, hakuona wafuasi wa Chadema waliokuwa kwenye mkutano huo uliyofanyika Februari 16,mwaka 2019 katika viwanja vya Buibui na Mwananyamala Kinondoni wakiwashambulia askari polisi.

Shahidi huyo alipoambiwa aeleze ni njia gani Mbowe aliitumia kuongoza mapambano ya kudai haki amedai kuwa yeye hafahamu ila mpelelezi ndiyo anafahamu njia aliyoitumia amedai kuwa ni sahihi.

Shahidi  alipoambiwa aeleze njia gani Mbowe aliitumia kuongoza mapambano ya kudai haki,amedai yeye hafahamu, lakini mpelelezi anafahamu njia aliyoitumia amedai kuwa ni sahihi Mbowe katika mkanda huo alitamka 'Hawataki fujo na hawatafanya fujo na hata kumuua inzi tunataka amani'.

Akiendelea kujibu maswali ya Kibatala, Koplo Charles alidai hajawahi kumpa mpelelezi wa kesi hiyo mkanda huo wa video ili autumie kuwahoji washtakiwa.

Akijibu swali la maandamano kuonekana kwenye mkanda huo, amedai unaonesha maandamano hayo kutoka uwanjani hadi Kinondoni Mkwajuni, ambapo aliishia kupiga picha hapo kutokana na fujo zilizokuwa zinaendelea.

"Nilikuwa napiga picha nikiwa kwenye gari la OCD na sijui kama kwenye gari hilo OCD alikuwepo, mimi dereva alinitoa tu pale na kunirudisha kituoni," alidai Koplo Charles

Akielezea kuhusu ni mshtakiwa gani kati ya hao aliyesema waandamane, amedai Mbowe ndiyo alihamasisha wafuasi hao waandamane.Pia, shahidi huyo amedai kuwa katika mkanda huo aliouonesha mahakamani hakumuonesha Mbunge wa Kawe Halima Mdee akiwahamasisha wafuasi hao kumpiga mawe Magufuli.

"Maneno aliyoyatoa Halima Mdee katika mkutano huo yalisababisha hisia za chuki dhidi ya wananchi, Rais na Serikali yao,lakini hajui kama kumchukia Rais ni kosa la jinai," amedai

Shahidi huyo alipoambiwa aeleze maneno ya uchochezi yaliyotolewa na viongozi wengine amedai hayakumbuki kwa sababu yaliongelewa kwa urefu, lakini amesisitinza kuwa walitamka maneno ya uchochezi na kuiomba Mahakama nafasi nyingine ya kuonesha mkanda huo kwa lengo la kujikumbisha.

Upande wa mashtaka uliwakilishwa na mawakili wa Serikali wa Kuu, Faraja Nchimbi, Dkt.Zainabu Mango na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon na Wakili wa Serikali, Jackline Nyantori.

Mbali ya Mbowe washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu Taifa, Dk. Vincent Mashinji , Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu Mkuu Taifa, Vicent Mashinji na Mbunge wa Kawe Halima Mdee.

Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kuwa, Februari 1 na 16, mwaka jana, Dar es Salaam waliku─║a njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post