KATIBU MKUU CCM DKT BASHIRU ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI AJALI YA MOTO MOROGORO


Na Stella Kalinga, Simiyu
Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Bashiru Ally ametoa salamu za rambirambi na kuwaombea majeruhi na waliofariki katika ajali ya moto Mkoani Morogoro, huku akitoa wito kwa wananchi kuwa zinapotokea ajali wawe wepesi wa kuokoa watu na mali za waliopata ajali badala ya kukimbilia kuchukua vitu ili kuepusha madhara.

Dkt. Bashiru ametoa salamu hizo wakati akizungumza na viongozi wa CCM wilayani Meatu katika kikao cha Ndani kilichofanyika Ukumbi wa CCM Mjini Mwanhuzi Agosti 11, 2019 ambapo amewaombea marehemu wote wapumzike kwa amani na majeruhi wapate afya njema ili waendelee na shughuli za ujenzi wa Taifa.

“Natoa pole kufuatia vifo vya wenzetu waliofariki katika ajali ya moto kule Mkoani Morogoro tuendelee kuwaombea waliotangulia  mbele ya haki wapumzike kwa amani na wale majeruhi waweze kupata afya na kurejea katika shughuli za kujenga Taifa”

“Kama Mwenyekiti wetu na Rais wetu alivyosema, tunapopata majanga kama haya ya ajali ni vizuri wote tuwe wepesi wa kuokoa waliopata ajali na mali badala ya kukimbilia kuchukua vitu kuepusha madhara makubwa”  alisema Dkt. Bashiru.

Akizungumza na Viongozi wa CCM wilayani Meatu, Dkt. Bashiru amewataka viongozi hao kutoa taarifa za watu wanao nunua pamba kwa njia ya Umachinga,  pasipo kutumia utaratibu unaotakiwa wa kupitia vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) kwa bei elekezi ya shilingi 1200/= ili waweze kuchukuliwa hatua.

Kwa upande wake  Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, maji na ujenzi huku akiwashukuru wabunge wa wilaya ya Meatu(Jimbo la Kisesa na Jimbo la Meatu) kwa namna wanavyojitoa binafsi na kupitia mifuko ya majimbo kuunga mkono juhudi za Serikali katika maendeleo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Meatu, Mhe. Salum Khamis amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. John Magufuli kukubali kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Draja la Sibiti ambalo ujenzi wake umerahisisha mawasiliano na utachangia katika kukua kwa uchumi wa wilaya ya Meatu, mkoa wa Simiyu na mikoa jirani.

Mara baada ya kuhitimisha kikao cha ndani na viongozi wa CCM Wilaya ya Meatu,  Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Bashiru Ally alipata fursa ya kutembelea na kuona ujenzi wa Daraja la Sibiti ikiwa ni ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ambapo alipongeza Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo linaiunganisha mikoa ya Simiyu na Singida.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Bw. Fabian Manoza amesema kutokana na ujenzi wa Daraja la Mto  Sibiti Halmashauri ina mpango wa kupanua stendi ya Mjini Mwanhuzi kwa kuwa magari mengi yameanza kupita Meatu kupitia daraja hilo.


MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527