JESHI LA POLISI KUIMARISHA ULINZI MKUTANO WA SADC

Jeshi la Polisi nchini limeeleza kuwa limejipanga kuimarisha ulinzi wakati wa Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika jijini Dar es Salaam.

 
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo kutoka Makao Makuu ya Polisi, Liberatus Sabas, alisema wamejipanga na tayari wameanzisha operesheni maeneo mbalimbali kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inaimarika wakati wote wa mkutano huo.

Mkutano huo umepangwa kufanyika kwa siku mbili kuanzia Agosti 17 na utahudhuriwa na wakuu wa nchi 16 wanachama.

Akizungumzia mkutano huo, Sabas alisema Jeshi la Polisi litahakikisha wageni wote wa mkutano huo watakuwa salama wakati wote wa mkutano na wanaondoka salama.

"Tumeanzisha operesheni maeneo mbalimbali kuhakikisha hali ya usalama inaimarika. Mikoa yote ambayo imepakana na Dar es Salaam na nchi kwa ujumla tutahakikisha inakuwa salama.

"Nitoe ujumbe kwa wahalifu, kama unafikiri hiki ni kipindi cha kujipatia, watajikuta wapo sehemu ambayo hawakuitegemea, watafute shughuli halali za kufanya wakati huu wa mkutano na siyo kujipanga kuja kujipatia vipato isivyo halali, wataishia mdomoni mwa simba.

"Ole wao watakaojaribu kwa maana tumejipanga vizuri, natoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa mbalimbali za matishio ya kihalifu, tunaahidi kwamba tutazifanyia kazi kwa haraka ili amani na utulivu uendelee," Sabas alisema.

Alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vyingine vya ulinzi na usalama wamejipanga kikamilifu kuimarisha ulinzi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527