JUMUIYA YA MADAKTARI WATANZANIA WALIOSOMA CHINA (DCAT) YATOA HUDUMA YA AFYA BURE KISARAWE, PWANI


WAKAZI wa Kisarawe wamenufaika na kambi ya kwanza ya kampeni ya uchunguzi na matibabu dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza inayotolewa na madaktari bingwa wa Jumuiya ya Madaktari  Watanzania waliosoma China (DCAT).

Awali akifungua kambi hiyo wiki hii katika Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo amewahamasisha kujitokeza kwa wingi ili kujua hali zao.

Jafo ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe ametumia fursa hiyo kuwasilisha ombi lake kwa Mwambata wa Ubalozi wa China, anayeshughulikia masuala ya utamaduni na elimu, Gao Wei, ambaye alimwakilisha Balozi wa China, kwamba waijengee Hospitali hiyo jengo la kisasa la matibabu.

"Tunashukuru wataalamu wetu wameona katika kampeni hii, Kisarawe iwe ya kwanza kisha watakwenda maeneo mengine ya nchi, Rais Dk. John Magufuli anatujengea jengo la kisasa la OPD (wagonjwa wa nje) hapa Kisarawe.

"Nitumie fursa hii kuuomba ubalozi wa China, ikizingatiwa pia kwamba Wilaya hii ina historia hasa katika ujenzi wa reli ya Tazara, Wachina walikaa hapa na wakazi wa Kisarawe walishiriki kuijenga.

"Ukiacha mahusiano yale ya ujenzi wa reli ya Tazara, leo hii wigo umepanuka mpaka kwenye elimu, afya na sekta nyinginezo," amesema.

Ameongeza "Nawasihi wakazi wa Kisarawe kuitumia fursa hii ya uchunguzi vizuri, hata yule mwenye mgonjwa aliyepo nyumbani amlete, hapa Wapo madaktari wabobezi watachunguzwa na watagundua tatizo linalomsumbua.

Kuhusu ombi hilo la Waziri Jafo, Mwambata huyo wa Ubalozi amesema amelipokea na kuridhia kwamba wapo tayari kujenga jengo la kisasa kwa Hospitali hiyo.

Awali, amesema ushirikiano wa China na Tanzania ni wa miaka mingi na imekuwa ikitoa ufadhili kwa watanzania kwenda kusoma nchini humo elimu mbalimbali .

Amesema wanafurahi kuona kwamba wataalamu waliopata ufadhili wa masomo China sasa wanasaidia nchi katika mambo mbalimbali.

Mwenyekiti wa DCAT, Dk. Liggyle Vumilia amesema katika siku hizo tatu wanatarajia kuwachunguza afya watu kati ya 600 hadi 1000 ambapo watachunguzwa magonjwa ya saratani, moyo, kisukari na mengineyo.

"Kampeni yetu ina kauli mbiu 'Jali Afya yako, Fanya uchunguzi mapema', tunalenga wananchi wa kawaida kabisa, kuwahamasisha wajenge tabia ya kuchunguza afya zao, itawasaidia kujua mapema kama wanakabiliwa na matatizo au la!

"Wale tutakaowakuta na matatizo madogo tutawatibu kupitia mfuko tulioandaa, tunawapa na elimu ya kujikinga dhidi ya magonjwa haya," amesema.

Amesema wanatarajia pia kwenda hivi karibuni mkoani Tanga ambako watafanya kampeni hiyo na baadae nchi nzima.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Jokate Mwegelo amesema utoaji wa huduma bora za afya ni miongoni kwa vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli na kwamba msisitizo zaidi ni katika utoaji wa huduma za kinga.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo  akiwashukuru wanajumuiya ya Watanzania walioishi nchini China (DCAT) kwa kujitolea kuwapa huduma ya afya bure kwa wakazi wa wila ya Kisarawe, Pwani. 
Picha zote na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo (kushoto) akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo  kutoa hotuba yake.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo amesema utoaji wa huduma bora za afya ni miongoni kwa vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli na kwamba msisitizo zaidi ni katika utoaji wa huduma za kinga.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Watanzania waliosoma nchini China Dkt. Liggyle Vumilia akielezea kwa ufasaha huduma hiyo ya afya bure.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Utamaduni wa Ubalozi wa China nchini Tanzania, Bwana Gao Wei akisoma hotuba yake.
Mtaalam wa Tiba ya jadi ya Kichina Dkt Paul Mhame akitoa ushauri kwa jamii.


Wananchi wa wilaya ya Kisarawe, Pwani na vitongoji vyake wakipima uzito na urefu ili kuweza kupatiwa matibabu ya bure kutoka kwa Jumuiya ya Madaktari  Bingwa Watanzania waliosoma nchini China (DCAT) waliopiga kambi kwa muda wa siku tatu. Jumuiya hiyo imejipanga kuendelea na zoezi la kutoa huduma katika mkoa wa Tanga na maeneo mengine ya Tanzania. Picha na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Dokta Bingwa wa Magonjwa ya Saratani, Dkt Heri Tungaraza akitoa maelekezo kwa wagonjwa.

Wagonjwa wakipimwa presha.
Wagonjwa wakipimwa ugonjwa wa Kisukari.
Mtatibu wa zoezi la upimaji wa Afya Bure, Bi. Linas akigawa maji kwa wagonjwa.

Wananchi wakisubiri huduma.
Wazee wakipatiwa ushauri kabla ya kuingia kuwaona Madaktari bingwa waliojitolea kufanya zoezi la kutoa huduma ya Afya Bure kwa wananchi wa Jumuiya ya Madaktari  Bingwa Watanzania waliosoma nchini China (DCAT).
Kila mmoja alijitahidi kumleta mgonjwa wake ili apatiwe huduma ya afya bure.
Wananchi wa wilaya ya Kisarawe, Pwani na vitongoji vyake wakipimwa presha ili kuweza kupatiwa matibabu ya bure kutoka kwa Jumuiya ya Madaktari  Bingwa Watanzania waliosoma nchini China (DCAT) waliopiga kambi kwa muda wa siku tatu.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Watanzania waliosoma nchini China Dkt. Liggyle Vumilia (aliyevaa tai) akitoa ushari kwa wagonjwa walifika kupatiwa huduma ya Afya bure iliyofannyika wilaya ya Kisarawe, Pwani.

Wananchi wa wilaya ya Kisarawe wakiwa wamepanga foleni kuoatiwa huduma ya Afya Bure.
Watoa huduma wakiendelea kutoa ushari kwa wagonjwa waliofika kupatiwa huduma ya Afya bure.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Watanzania waliosoma nchini China Dkt. Liggyle Vumilia akigawa maji kwa wagonjwa aliojitokeza kupatiwa huduma ya Afya Bure.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527