Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga Awasili Mkoani Simiyu, Aridhishwa Na Maandalizi Ya Nanenane Kitaifa

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga tarehe 29 Julai 2019 amewasili Mkoani Simiyu kwa ajili ya kujionea maandalizi ya Maadhimisho 26 ya sikukuu ya wakulima maarufu kama (Nane Nane) yenye lengo la kuwatambua na kuwaenzi Wadau Wakuu wa Sekta ya Kilimo ambao ni Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika, Wasindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili kwa mchango wao mkubwa wanaoutoa katika kuendeleza uchumi wa nchi yetu.

Mwaka huu wa 2019, sherehe hizi zinafanyika Kitaifa mjini Bariadi katika Viwanja vya maonesho ya kilimo Nyakabindi katika Mkoa wa Simiyu hivyo Mhe Hasunga amepongeza Uongozi wa mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara kwa juhudi zao za kufanikisha kuingiza uwanjani huduma za msingi ambazo ni maji na umeme.

Alisema kuwa jukumu hilo kwa Serikali na Wadau wa Sekta Binafsi ni kuendeleza viwanja hivyo vya Nyakabindi kwa kujenga mabanda ya maonesho ya kudumu na kuboresha huduma muhimu za kijamii ili kuwe na maonesho endelevu yenye sura ya Kitaifa na Kimataifa.

Alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali, imeendelea kuongeza na kuboresha viwanja vya maonesho katika Kanda mbalimbali hapa nchini, kwa sasa kuna viwanja nane (8) vya maonesho ya kilimo ambavyo ni Themi (Arusha) Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara;  Mwl. J.K.Nyerere (Morogoro) Kanda ya Mashariki ambayo mikoa yake ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Tanga;na John Mwakangale (Mbeya) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Katavi, Songwe na Rukwa;

Vingine ni Nzuguni (Dodoma) katika Kanda ya Kati yenye mikoa ya Dodoma na Singida; Nyakabindi (Bariadi) Kanda ya Ziwa Mashariki yenye mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara; Nyamuhongolo (Mwanza) Kanda ya Ziwa Magharibi yenye mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita; Ngongo (Lindi) Kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Mtwara na Lindi na Fatma Mwasa (Tabora) Kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Tabora na Kigoma.

Akizungumza na mtandao wa Wazo Huru Blog, Waziri huyo wa kilimo ameeleza kuwa Wakati wa sherehe hizo za Nane Nane, Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika na Wadau wengine katika Sekta za Kilimo; watapata fursa nzuri zaidi ya kuona na kujifunza mbinu na teknolojia sahihi za uzalishaji na usindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, maliasili na bidhaa nyinginezo kupitia Maonyesho ya Kilimo yanayoandaliwa.

Aidha, kwa Wafanyabiashara itakuwa ni fursa nzuri ya kutangaza bidhaa zao hususani pembejeo na zana mbalimbali za uzalishaji na usindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili.

Aliitaja Kaulimbiu ya sherehe za Nane Nane Mwaka huu ni kuwa ni “Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ukuaji wa Uchumi wa Nchi”.  Kaulimbiu hii imechaguliwa baada ya kutafakari kwa undani suala zima la Uchumi wa Viwanda unavyoweza kuchangia katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, pato la Taifa na wakati huo huo kupambana na Umaskini.

"Ni ukweli ulio dhahili kuwa Kilimo ni Sekta kubwa na muhimu kwa maendeleo kutokana na mchango wake katika uchumi wa Taifa. Mfano katika mwaka 2017, Sekta ya Kilimo ilitoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 65.5, ikichangia asilimia 28.7 ya pato la Taifa. Sambamba na hilo Sekta ya Kilimo inachangia asilimia 65 ya malighafi za viwandani. Takwimu zinaonesha kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2018 ukuaji wa Sekta ya Kilimo ulifikia asilimia 7.1" Alikaririwa Mhe Hasunga

Ameongeza kuwa Kaulimbiu ya mwaka huu inahamasisha Wakulima, Wafugaji, Wavuvi na Wanaushirika kuleta mapinduzi katika Sekta za Kilimo kwa kuzalisha kwa tija ili kukuza uchumi wa Mkulima, Mfugaji, Mvuvi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Kadhalika, ametoa wito kwa Wananchi na Wadau wote kushiriki kikamilifu na kuhudhuria kwa wingi maonesho hayo kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti, 2019.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments