WAZIRI LUGOLA, ZUNGU WAFANYA OPERESHENI KUWASAKA MATEJA BONDE LA JANGWANI , RPC ILALA APEWA AGIZO ZITO


Na Felix Mwagara, MOHA.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amefanya operesheni ya kuwasaka na kuwakamata mateja mbalimbali ambao wanatumia dawa za kulenya na kufanya uhalifu katika bonde la Jangwani, Ilala, jijini Dar es Salaam.

Lugola ambaye aliongozana na Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azan Zungu, kuwasaka mateja hao ambao wanatumia aina mbalimbali ya madawa ya kulenya, baada ya kuona viongozi hao wanawasaka walikimbia katika maeneo ya vijiwe vyao.

Waziri Lugola wakati akiwa katika operesheni hiyo ambayo ilidumu kwa saa moja na nusu kwa kutembelea mitaa mbalimbali ya bonde hilo, alimpigia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala-RPC, ACP Zuberi Chembera, kufika katika eneo hilo huku akiwa na askari kwa ajili ya kuendeleza zoezi hilo.

Akizungumza na wananchi wa Kata hiyo ya Jangwani, leo, Waziri Lugola alisema wahalifu hawa wanapaswa kusakwa kwa nguvu zote na kukamatwa, kwasababu walishampora mtu katika mitaa hiyo na kumuaa.

“RPC kuanzia muda huu, nakuagiza askari wako waingie mitaani, kuwakamata wahalifu hawa, na nitakuja saa 12 jioni ya leo, kuona wahalifu wote katika bonde hili wamejaa katika kituo cha Msimbazi, na muwakamate wahalifu na sio kuwaonea watu wasiokuwa na makossa,” alisema Lugola.

Lugola aliongeza kuwa, Serikali haiwezi kukaa kimya kufumbia macho matukio ya kiuhalifu ambayo yamekithiri katika eneo hilo na kuwafanya wananchi kutopata usingizi kuhofia kuvamiwa kwa muda wowote usiku au mchana. Alimtaka Kamanda wa Polisi Mkoa huo, kuendelea kufanya operesheni ya mara kwa mara kuwasaka wahalifu hao ambao wengi wao ni mateja ambao wanatumia dawa za kulevya.

Kwa upande wake Mbunge Zunge, ambaye ndio alimwita Waziri huyo kutembelea eneo hilo kuona kero kubwa awanazopata wananchi wake, alisema wahalifu hao hawatoki pekee katika Jimbo lake, bali wengi wao wanatoka maeneo mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam.

“Wenyeji wa eneo hili ni wachache, wengi wanatoka mitaa mbalimbali ya hapa Dar es Salaam ikiwemo Temeke na kwingineko, hivyo mheshimiwa Waziri tunajua utendaji wako, tunakuomba hii kero inatuumiza sana, wananchi wanakosa amani kutokana na uwepo mkubwa wa wahalifu hawa,’ alisema Zungu.

Waziri Lugola alisema Dkt John Magufuli anawataka wananchi wake waishi kwa amani na utulifu, yeye Waziri hatakubali kuona matukio hayo ya baibu yakishika kasi mitaani. Aliwataka Makamanda wa Polisi nchini kuwasaka wahalifu muda wowote si mpaka yeye atoe agizo au atembeleee.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527