ALICHOKISEMA BASHE BAADA YA KUTEULIWA KUWA NAIBU WAZIRI


Naibu Waziri wa Kilimo mteule, Hussein Bashe ameahidi kuiboresha sekta ya kilimo kwa kuwa ndiyo sekta iliyoajiri Watanzania wengi na kuchangia pato la taifa kwa asilimia kubwa licha ya changamoto nyingi.

Aidha, amemshukuru Rais Magufuli kwa kumteua kushika nafasi hiyo. Bashe ameteuliwa kushika nafasi hiyo leo Jumapili Julai 21, akichukua nafasi ya Innocent Bashungwa mbaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter leo saa chache baada ya kuteuliwa, Bashe ameandika ujumbe wa shukrani kwa Rais Magufuli akishukuru kwa kumteua na ameupokea uteuzi huo.

“Ndugu zangu awali nimshukuru Allah kwa yote , namshukuru kwa dhati Mh Rais kwa Imani yake, ni jukumu zito nimelipokea kwa uwezo wa Allah tutavuka ni ‘sector’ iliyoajiri Watanzania wengi na changamoto nyingi nawashukuru Watanzania, wananchi wa Nzega na kwa dhati chama changu,” ameandika Bashe.

Aidha, pamoja na uteuzi huo wa Bashe, Rais Magufuli pia amemteua aliyekuwa Waziri wa Tawala za Mikoa (Tamisemi), George Simbachawene kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, akichukua nafasi ya January Makamba ambaye uteuzi wake umetenguliwa.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527