VIJANA WAPEWA ELIMU KUHUSU KUANZISHA BIASHARA ILI KUJIKWAMUA NA UCHUMI


Na.Mwandishi Wetu-DSM
Vijana wamepewa elimu kuhusu kuanzisha biashara ili kujikwamua na uchumi kwa  kuchangamkia fursa zilizoko kwenye maeneo yao na kujua umuhimu wa kodi katika biashara ili kuwezesha taifa kupata mapato na wao kupata faida. 


Akizungumza katika Semina ya Vijana iliyoandaliwa na Umoja wa Vijana Tanzania (TYVA), Afisa Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi kutoka TRA, Isihaka Sharifu alisema kuwa Serikali imerekebisha baadhi ya Sheria za kodi hususani kwa vijana wanaofungua kampuni au biashara mpya. 


Sharifu alisema kuwa kwa sasa Sheria ya kodi imejikita kuwasaidia vijana wanaoanzisha kampuni na biashara mpya kwani imeweza kugusa msamaha wa kodi kwa miezi sita tofauti na awali ambapo biashara mpya zilikuwa zinalipiwa kodi baada ya miezi mitatu. 


“ Kwa sasa Sheria inasema ukiwa unafungua biashara yako au kampuni mpya kwa sasa unatakiwa kulipa kodi baada ya miezi sita, kwa hiyo hii itawasaidia vijana wengi ambao wanania ya kuanzisha biashara, nawasihi vijana wenzangu tumieni Fursa hiyo kujikwamua kiuchumi”, Alisema Sharifu. 


Katika Semina hiyo ambayo kauli mbiu yake ilikuwa ‘Nguvu ya Kodi’ Sharifu alipaeleza kuwa TRA inatekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kuwakwamua vijana hasa wajasiriamali wadogo ambao wanafanya biashara zao kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini. 


Alisema kuwa kodi inayotozwa kwa wafanya biashara wenye mauzo kuanzia milioni 0 hadi 100 imegawanyika katika makundi manne ambayo ni mauzo kuanzia 0 mpaka milioni 4 ambao hawatozwi kodi, mauzo ya milioni 4 mpaka 7.5 wanatozwa 100,000, milioni 7 mpaka 11 wanatozwa  250,000 na milioni 11 mpaka 14 wanatozwa 450,000 tofauti na hapo zamani ambapo walikuwa wanatozwa 546,000, kwa hiyo vijana wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo. 


Kwa upande wake, Afisa Vijana kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Anna Marika alisema kuwa vijana wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kutimiza wajibu wao kwenye suala la kulipa kodi kama Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. John Pombe Magufuli anavyoagiza. 


“Nimefurahi kwa Semina hii kwani watoa mada wamekuja na Mada nzuri zinazoelimisha ulipaji Kodi, wito wangu kwa vijana ni kwamba wanatakiwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kama Rais alivyoagiza kuchukua vitambulisho ili wasipate shida kwenye maeneo yao ya kufanyia Biashara”, Alisema Marika. 


Marika aliongeza kuwa kwa Wilaya ya Temeke wamejikita zaidi katika kuwasaidia vijana, wanawake na walemavu kujikwamua kimaisha kama Ofisi ya Rais –TAMISEMI ilivyoagiza kuwa asilimia 10 ya mapato ya halmashauri ijikite kwenye kuwasaidia vijana, wanawake na walemavu. 


Alisema Wilaya ya Temeke imetanga asilimia nne kwa vijana, asilimia  nne kwa wanawake na asilimia mbili kwa walemavu, huku wakilenga kuboresha utoaji wa huduma kwa kutoa vifaa vya kazi kwa vikundi mbalimbali kama vile pikipiki, Chelehani,vifaa vya mziki na magari ya kuzoa takataka na kusomba matofali. 


Alitolea mfano wa kikundi cha wanawake waliopewa chelehani 50 na wataanza kurejesha mikopo baada ya miaka miwili na wakimaliza mkopo vifaa vile vinakuwa mali ya kikundi. 


“Niombe sasa kwa wale vijana ambao mnaisha Temeke, haijarishi unatoka Wilaya gani hapa Dar es Salaam au mkoani, mkirudi kwenu kachangamkieni fursa hii ili kuwawezesha kujikimu kimaisha na kupata faida kubwa ya kuendesha uchumi wenu”, Alisistiza Marika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post