RC MAHENGE AIAGIZA TIRA KUFUATILIA KAMPUNI ZA BIMA ZINAZONYONYA HAKI ZA WATEJA

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

Mkuu wa Mkoa Wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge  ametoa agizo  kwa  Mamlaka ya Usimamizi  wa Bima[TIRA] kwa kanda ya kati Kuhakikisha inafuatilia na kuzichukulia hatua za kisheria  kampuni za Bima ambazo   zimekuwa zikiharibu utoaji wa huduma  kwa wananchi.

Dokta Mahenge ametoa agizo hilo Julai 18,2019  wakati wa ufunguzi siku ya  maadhimisho ya Bima kwa kanda ya kati ambayo imeanza Julai 17 hadi 19,2019  yakifanyika katika viwanja vya Nyerere  Square jijini  Dodoma.

Dokta Mahenge amebainisha kuwa pamekuwepo na changamoto kwa  baadhi ya makampuni  ya Bima kushindwa  kutoa huduma ipasavyo  na kutotoa huduma  ya fidia kwa wakati ,kwa wateja na badala yake yamekuwa yakitoa  huduma hafifu huku lengo lake ni kunyonya haki zao pindi wanapokumbwa na majanga licha  ya kuwa na vigezo vyote hivyo Wakati umefika sasa kwa Mamlaka ya usimamizi wa Bima[TIRA]kuzichukulia hatua kampuni kama  hizo.

“Kuna  baadhi ya kampuni za bima badala ya kutoa huduma bora kwa wananchi zimekuwa kilio,mfano  mwananchi analipia kila kitu kwenye kampuni ya bima lakini anapopata majanga aidha ajali majanga ya moto inachelewesha kumpa fidia ,hivyo niagize TIRA ifuatilie suala hili ambalo imekuwa kero kwa wananchi.Kampuni moja ya bima ikiwa chafu imeharifu taswira  ya makapuni mengine pia”alisema Dokta Mahenge.

Aidha,Dokta Mahenge amesema Tasnia ya Bima ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi endapo itaendeshwa kwa kufuata miongozo na taratibu ya kisheria huku akitoa wito kwa makampuni ya bima kuendelea kutoa elimu kwa wananchi umuhimu wa bima hivyo ni wajibu kwa makampuni ya bima kutoa huduma nzuri  na yenye viwango ili kuvutia wawekezaji makao makuu ya nchi,Dodoma.

Hata hivyo,Dokta Mahenge amesema ni Muhimu kwa makapuni yote ya Bima yakatoa huduma ya Bima ya Afya huku akitanabaisha kuwa serikali imeongeza bajeti  ya dawa hospitalini kutoka Milioni 900 hadi  Bilioni 4 kwa Mkoa wa Dodoma.

Kwa  upande wake,Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi  wa Bima[TIRA]Kanda ya kati  Bi.Stella Rutagiza  amesema  mwaka 2015 serikali ilianzisha ofisi ya Msuluhishi wa  Migogoro ya Bima Tanzania[Tanzania Insurance Ombundsmen] ambayo inaongozwa na Jaji Mstaafu Mhe.Vicent Lyimo ikiwa na lengo la kuwasaidia wananchi wake wenye  migogoro  ya Bima ili kuepuka gharama kubwa za kwenda mahakamani.

Aidha,Bi.Stella ametaja baadhi ya madhumuni ya maadhimisho ya siku ya Bima kanda ya kati kuunga mkono  juhudi kubwa za Rais  Mhe.  John Pombe Magufuli kuinua uchumi wa nchi,kutoa elimu pamoja na kupanua wigo wa huduma za Bima.

Katika hatua nyingine Bi.Stella amebainisha baadhi ya Mafanikio ya TIRA ni pamoja na kuongezeka  watoa huduma za Bima kutoka 10 mwaka 2015 na kufikia watoa huduma 27 mwaka 2019 pamoja na kupungua kwa malalamiko ya Bima kutoka kwa wananchi ambapo mwaka 2017kulikuwa na malalamiko 17,mwaka 2018  malalamiko 13  na kupokea malalamiko  matatu pekee kwa mwaka 2019.

Maadhimisho ya siku ya Bima kanda ya kati  tarehe  17-19/2019  yanaenda sambamba na kaulimbiu isemayo”Kata Bima,Inua Uchumi wa Nchi Yako”


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527