RAIS MAGUFULI AFURAHISHWA NA UJIO WA RAIS KENYATTA NCHINI


Na: Frank Shija – MAELEZO, Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kuwa Rais wa kwanza wa nje kutembelea Wilaya ya Chato.

Amesema kuwa ukiachilia mbali ujirani uliopo baina ya Tanzania na Kenya, pia kuna undugu kwa kuwa tunazungumza lugha moja, tunamuingiliano wa kijamii ikiwemo kuoana na kuwa na utamaduni unaofanana.

“Kufika kwako umeudhihirishia umma wa dunia kuwa sisi ni majirani, na marafiki wa kweli siku zote tutatembea pamoja kamwe tusikubali kulaghaiwa na watu,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema kuwa kutokana na ushirikiano huo wafanyabiasha wa Kenya na Tanzania wamekuwa wakishirikiana katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kijamii ikiwemo kuwekeza katika nchi zetu.

Kwa ujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Kenya imewekeza miradi 504 yenye thamani ya dola 1.7 biloni ikiwa na idadi ya watu 50,956 huku wawekezaji wa Tanzania nchini Kenya wakiwa wakekezaji 24.

Aidha katika Sekta ya Utalii, Tanzania ni nchi ya pili kwa watu wake kutembela nchini Kenya ikitanguliwa na nchi ya Marekani ambapo kwa mujibu ya takwimu za Bodi ya utalii ya Kenya ya Mwaka 2018 Watanzania 222,216 walitembelea Kenya ambayo ni zaidi ya 10% ya watu wote waliotembelea Kenya.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli ameitaja miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa kwa ushirikiano wan chi hizi mbili ikiwemo barabara ya Holili- Arusha hadi Namanga pamoja na maandalizi ya ujenzi wa Barabara kutoka Mombasa hadi Bagamoyo.

Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania ipo katika hatua mbalimbali za kujenga meli tano ambapo itaanzisha safari za kutoka Bukoba – Mwanza – Kisumu na Jinja.

Vile vile Rais Dkt. Magufuli ametoa wito kwa wawekezaji kutoka Kenya kuja kuwekeza nchini hapa kwa kuwa milango ipo wazi kwa mwekezaji yeyote na Watanzania waendelee kuwekeza Kenya ili kuendeleza ushirikiano uliopo kwa mustakabari wa maendeleo ya nchi zote mbili.

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyata amesema anayofuraha kuwa Rais wa kwanza wa nje kukanyaga ardhi ya Chato.

Ameongeza kwamba uwepo wake Chato Mkoani Geita ni udhibitisho kuwa nchi hizi ni ndugu na wapo kwa ajili ya kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Kenya.

“Hakuna mtu anayeweza kututenganisha kamwe, sisi kama watu wa Afrika Mashariki yatupasa kuhakikisha tunaondoa vikwazo vyote vitakavyozuia kutembeleana, kufanyabiashara pamoja na pengine hata kuoana.” Alisema Kenyatta.

Apongeza Ujenzi Uwanja wa Ndege Chato
Rais Kenyatta ameipongeza Serikali kwa kujenga uwanja wa ndege wa Chato kwa kuwa ni utaimarisha na kukuza ukuaji wa biashara na shughuli nyingine za kimaendelea katika ukanda huo jambo ambalo halipaswi kubezwa.

Amesema anashangazwa na baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakipuuza jitihada hizo za kujenga uwanja huo kwani ni muhimu na yeye kama Rais wa Kenya angependa kuona Afrika ya Mashariki inakuwa kitu kimoja.

Amechukizwa na kauli za baadhi ya wanasiasa na kusema haiwezekani kumzuia Mtanzania kufanya biashara au kuoa nchini Kenya vivyo hivyo kwa Wakenya nchini Tanzania.

Rais Kenyatta yupo hapa nchini ikiwa ni ziara yake binafsi kwa siku mbili kuanzia leo tarehe 05 Julai hadi siku ya kesho Jumamosi ya tarehe 06 Julai 2019.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527