KESI YA KUPINGA SHERIA YA NDOA YAUNGURUMA


Rufaa ya kesi ya kupinga sheria ya ndoa ya mwaka 1971, iliyofunguliwa na Mkurugenzi wa taasisi ya Msichana Initiative Rebecca Gyumi, leo Julai 24 imeanza kusikilizwa katika mahakama ya Rufani ya Tanzania.

Katika kesi hiyo ambayo Serikali ilikata rufaa baada ya upande wa mashtaka kushinda, Wakili wa Serikali Mkuu Mark Mlwambo, amesema sheria ya ndoa ya mwaka 1971, haina madhara kwa mtoto wa kike na inapaswa kuendelea kutumika.

Akizungumza mbele ya jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, wakiongozwa na Jaji Augustine Mwarija, Wakili wa upande wa mashtaka Jebra Kambole, amesema Sheria hiyo ni kandamizi, inadhalilisha na kuchochea ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake Rebecca Gyumi amezibainisha sababu zilizomsukuma kupinga sheria hiyo.

''Nilifungua kesi hiyo kwa sababu ya ukweli kuwa, suala la watoto wa kike kuolewa kabla ya umri limekuwa ni kubwa sana katika nchi yetu na ukiangalia takwimu mbalimbali zinazoongelea ndoa za utotoni zinaeleza kuwa, wasichana wawili kati ya watano wanaolewa kabla ya kufikisha miaka 18'' amesema Rebecca Gyumi.

Rebecca ameongeza kuwa, ndoa za utotoni ni ndoa ambazo zimekuwa zikiwaletea athari za kiafya na kielimu mabinti wengi, kwani hushindwa kutimiza ndoto zao na kwamba alifungua shauri hilo ili kuangalia ni namna gani, itaweza kuondoa ubaguzi wa umri wa mtoto wa kike kuolewa pamoja na kulinda maslahi mapana, yaliyopo kati ya mtoto wa kike na wa kiume.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527