Picha : WIZI MPYA WA DHAHABU WAIBULIWA SHINYANGA...WAZIRI BITEKO ATOA MAAGIZO MAZITO

Na Salvatory Ntandu - Malunde 1 blog Kahama

Serikali imesema itachukua hatua kazi za kisheria kwa Wanunuzi wa madini watakaobainika kununua madini nje ya masoko yaliyotengwa ikiwemo kutaifisha mali zote atakazo kamatwa kutokana na baadhi yao kutotii sheria za nchi katika biashara ya madini.

Hayo yamebainishwa leo Julai 17,2019  na Waziri wa Madini,Mhe. Dotto Biteko wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wachimbaji na wanunuzi wa madini katika kijiji cha Kakola kilichpo katika halmashauri ya Msalala na kubaini utoroshwaji wa madini.

Amesema ofisi yake imepata taarifa za kuwepo kwa wanunuzi 12 wanaonunua dhahabu katika eneo hilo bila yakuwa na vibali huku wengi wao wakiitorosha kwenda kuiuza katika nchi za Kenya na Uganda na kuikosesha serikali mapato huku maafisa wake wakikaa kimya.

Katika ziara ya kushitukiza aliyoifanya leo Biteko amebaini wizi huo mpya ambao unatumiwa na wafanyabiashara hao kwa kununua dhahabu kwa wachimbaji wadogo huku wao wakigoma kuipeleka katika masoko rasmi.

Amesema kitendo hicho ni cha kuihujumu nchi kwa kununua dhahabu katika masoko ambayo hayatambuliwi na serikali huku serikali ikiendelea kukosa mapato licha ya kuwa imepunguza kodi katika sekta ya madini kutoka asilimia 17 hadi asilmia 7.

Waziri Biteko amesema wamembaini Mnunuzi mmoja ambaye amenunua wa dhahabu kilo tatu katika kijiji cha Kakola yenye thamani ya shilingi Milioni 300 lakini mrahaba hakuweza kulipia hawezi kulipa kutokana na kununua kinyemela.

Amesema Mnunuzi wa pili alinunua dhahabu kwa muda wa wiki mbili na alipata kilo 2.64 na kuuza kiasi cha shilingi Milioni 241 pia nae hakuweza kulipa mrahaba wa serikali.

Naye Kamishina wa Tume ya madini, Prof.Abdulkari Mruma amesema serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watumishi wa ofisi ya madini watakaobainika kuhusika katika njama hizo kwani tatizo hilo wanalifahamu lakini hawakutoa taarifa kwa mamlaka husika.

“Haiwezekani sisi tutoke wizarani tuje tukamate wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi pamoja na viwanda (Elution plant) ilivyofungwa na serikali ikiendelea kufanyakazi bila kufunguliwa huku maafisa madini wakiwa wamekaa kimya”alisema Mruma.

"Tumebaini Plant iliyofungwa na Ofisi ya madini ikeendelea kufanyakazi bila kibali kutoka serikalini huku viongozi wa ofisi ya madini wakiwa hawana taarifa jambo ambalo linatiashaka juu ya utendaji kazi wao hivyo wanapaswa kubadilika na kujitathini katika nafasi zao",alisema.
Waziri wa Madini,Mhe. Dotto Biteko akizungumza katika mkutano wa hadhara na wachimbaji na wanunuzi wa madini katika kijiji cha Kakola kilichopo katika halmashauri ya Msalala na kubaini utoroshwaji wa madini.Picha zote na Salvatory Ntandu - Malunde1 blog
Waziri wa Madini,Mhe. Dotto Biteko akizungumza katika mkutano wa hadhara na wachimbaji na wanunuzi wa madini katika kijiji cha Kakola kilichopo katika halmashauri ya Msalala 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527