DR. BASHIRU: WAPUUZENI HAO "WAPUMBAVU" WANAOTAKA KUKIVURUGA CHAMA CHETU


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dkt. Bashiru Ally,  leo Julai 23,  2019,   ametoa wito kwa wanachama wa chama hicho kuwapuuza wale aliowaita wapumbavu, yaani watu wanaoendeleza mjadala usiokuwa na tija ndani ya chama hicho, na akawahakikishia kwamba chama hicho kiko imara.


Dk. Bashiru  ameyasema hayo wakati akipongeza hatua ya wanaCCM Mkoa wa Dodoma, kutaka Kanal Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba, makatibu wastaafu wa CCM kuchukuliwa hatua.

Ni baada ya makatibu hao wastaafu wiki iliyopita, kumwandikia barua Pius Msekwa, Katibu wa Baraza la Viongozi Wastaafu wa CCM wakilalamikia kuchafuliwa na Cryspian Musiba, anayejitambulisha kuwa mtetezi wa Rais John Magufuli.

Kwenye barua hiyo, Makamba na Kinana wamelalamika kuchafuliwa na kuzushiwa huku serikali ikishindwa kuchukua hatua. Hata hivyo, wamehoji ‘ulinzi’ anaopewa Mtu huyo  anayewachafua.

Akizungumza tamko lililotolewa na Halmashauri ya CCM Mkoa wa Dodoma jana, Dk. Bashiri amewataka makada wa chama hicho kuwapuuza ‘wapumbavu’ hao.

“Wapuuzeni hao wapumbavu, hatuogopi kukosolewa, lakini hatuko tayari kudharauliwa, kutukanwa na kubezwa na majina yaliyo na kebehi na watu wasio na shukrani. Hatujafunzwa hivyo, hatujazoea hivyo,” amesema Dk. Bashiri bila kutaja jina lolote.

Aidha, Dk. Bashiru amesema, uongozi wa CCM hautaruhusu malumbano ndani ya chama hicho, huku akieleza kwamba mwenyekiti wake, Dk. Magufuli yuko tayari kuwasamehe, ili kukijenga chama.

“Msijifanye majasiri wa kupambana na malumbano, hakuna ruksa hiyo kwenye chama chetu. Waacheni wabwabwaje kitoto toto watachoka wenyewe.



"Ole wake mwanaCCM yeyote atakayetaka kutumia fursa ya upumbavu wa wapumvavu wa mwaka kutafuta kiki, ya kisisasa ili achaguliwe kwenye seriali za mtaa, hapana msifanye hivyo.


 “Jifunzeni kutoka kwa kiongozi wetu ambaye wakati wote hana muda wa malumbano. Amevumilia, wanaomtusi wengine wana umri wa watoto wake amewavumilia na yuko tayari kuwasamehe pia.  Lakini kwa kufanya hivyo si kwamba ni muoga.


“Mwalimu Julius Nyerere alishatuhasa tujisahihishe, kujisahihisha ni kujiimarisha, tujikosoe, tukosoane kwa adabu kwa nidhamu tuache utoto. Kisiwe chama cha siasa za kipuuzi, sababu majira haya ni ya uchaguzi,” amesema Dk. Bashiru.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527