IGP SIRRO AAGIZA UCHUNGUZI UFANYIKE AJALI ILIYOUA WAFANYAKAZI WA AZAM TV

Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Tanzania (IGP), Simon Sirro ameagiza kufanyika uchunguzi kubaini chanzo cha ajali ya magari mawili iliyotekea eneo la Shelui mkoani Singida na kusababisha vifo vya watu saba wakiwemo wafanyakazi watano wa kampuni ya Azam Media (pichani).

Akizungumza jijini Mwanza leo Jumatatu Julai 8, 2019 katika ziara yake ya kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba za polisi eneo la Myamhongolo, IGP Sirro ameuagiza uongozi wa jeshi hilo mkoani Singida kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayebainika kuwa chanzo cha ajali hiyo iliyojeruhi wafanyakazi wengine wa kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa uzalishaji vipindi wa kampuni ya Azam Media, Yahya Mohamed, waliofariki dunia katika ajali hiyo iliyotokea asubuhi ya leo ni Salim Mhando, Florence Ndibalema, Said Haji, Sylvanus Kasongo na Charles Wandwi.

Madereva wa Coaster lililokuwa limewapakia wafanyakazi 10 wa kampuni hiyo, pamoja na dereva wa lori pia wamefariki katika ajali hiyo iliyotokea wakati wafanyakazi hao wakiwa njiani kwenda wilaya ya Chato Mkoa wa Geita nchini Tanzania kuripoti tukio la uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Chato-Burigi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post