VIJANA MIKOA SABA TANZANIA WAKUTANA SHINYANGA KWENYE KONGAMANO LA JUMUIYA YA WAISLAM WA AHMADIYYA

Vijana hapa nchini wametakiwa kubadilika na kuachana na vitendo vinavyomchukiza Mwenyezi Mungu ambavyo ni pamoja matumizi ya dawa za kulevya, wizi, na uasherati, ambavyo vinaweza kubabisha wakapoteza mwelekeo na kutotimiza malengo yao.


Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili Julai 7,2019 na Kiongozi wa Vijana wa Kitaifa wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya, Sheikh Ramadhan Hassan Nauja katika kongamano la siku tatu lijulikanalo kama Ijtemaa ya Khuddam Kanda ya Kaskazini la Mwaka 2019 linalojumuisha washiriki kutoka mikoa saba lililofanyika katika wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Sheikh Nauja amesema ipo haja kwa viongozi wa dini kuhakikisha wanawalea vijana katika misingi ya kiimani ambayo itawasaidia kupata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kuwa raia wema katika maeneo wanayoishi.

Amesema vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa hivyo ni budi kwa viongozi wa dini wakawajengea misingi mizuri ya kumjua Mwenyezi Mungu na kuondokana na vitendo viovu kwani ndiyo kundi pekee ambalo lipo katika hatari kubwa ya kukumbwa na vishawishi katika ulimwengu huu.

Naye Sheikh Musa Issa kutoka Visiwani Zanzibar amesema viongozi wa dini wanapaswa kujikita kutoa elimu ya dini kwa wananchi waliopo vijijini ili kuwasaidia kumjua Mungu na kuondokana na matukio ya mauaji ya vikongwe na ulawiti na watu wenye ualbino.

Kwa upande wake, Sheikh Yusuph Mgeleka kutoka Kahama amesema Kongamano hilo litasaidia  kuwabadili vijana kifikra na kuwa raia wema kwa kufanya kazi halali ambazo zitaweza kuwapatia vipato na kuongeza nguvu kazi katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mahdilah Issa na Musa Saidi ambao ni miongoni mwa washiriki  kongamano hilo kutoka mikoa ya Tabora na Kagera,wamesema mafunzo waliyoyapata yatawawezesha kuwa mabalozi kwa vijana wenzao katika maeneo yao wanayoishi ili kutoa fursa ya vijana wengine.

Kongamano hilo limejumuisha vijana zaidi ya 200 kutoka katika mikoa ya Tabora, Mwanza, Kagera, Geita, Simiyu na Mara limeenda sambamba na mashindano ya Kusoma Quran Tukufu,mashindano ya mpira wa miguu na shughuli mbalimbali za kijamii katika mji wa kahama na lilianza rasimi siku ya Ijumaa na limehitimishwa leo Jumapili.
Na Salvatori Cevin - Malunde1 blog
ANGALIA PICHA
Viongozi wa kitaifa wa Jumuiya ya kiislama ya Ahmadiya wakiomba dua kabla ya kuanza kwa kongamano hilo. Picha zote na Salvatori Cevin - Malunde1 blog
Kiongozi wa Vijana wa Kitaifa wa Jumuiya ya Waislam wa (Ahmadiya) Shekh, Ramadhan Hassani Nauja kushoto akisoma dua katikati ni Sheikh, Musa Issa kutoka Visiwani Zanzibar kulia ni Sheikh Yusuph Mgeleka.
Viongozi mbalimbali wa Kongamano hilo wakiwa wanasikiliza kwa makini mada zinavyowasilishwa.
Shekh Yusuph Mgeleka akiwasilisha mada mbalimbali katika kongamano hilo.
Shekh, Musa Issa kutoka Zanzibar akisoma Quan Tukufu katika kongamano hilo ambalo lilikuwa na mashindano ya kusoma kitabu hicho.
Washiriki wa kongamano hilo la siku tatu liliofanyika mjini Kahama.
Viongozi mbalimbali wa jumuiya ya kiislam ya ahmadiya kutoka mkoa wa shinyanga wakiwa na viogozi wa kitaifa wa jumuiya hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527