WATUMISHI MWAUWASA WATAKIWA KUSHIRIKIANA


Watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) wametakiwa kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu yao na kufanya kazi kwa uadilifu.

Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga alitoa wito huo hivi karibuni wakati wa mkutano na wafanyakazi wote uliofanyikia kwenye ukumbi wa Mikutano wa Mamlaka kwenye jengo la Maji House ikiwa ni utaratibu aliyojiwekea wa kuzungumza na watumishi wote kila mwezi.

Mhandisi Sanga alisema ili kupata matokeo chanya, watumishi wote hawana budi kuhakikisha wanafanya kazi kwa uadilifu na wanakuwa kitu kimoja na kwamba yampasa kila mtumishi kutambua na kuheshimu nafasi ya mwenzake kwenye utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

“Hakuna mtumishi aliyebora kumzidi mwenzake, sote tunahitajiana ili kutimiza majukumu yetu na ndiyo maana kukawa na mgawanyo wa majukumu. Yatupasa tufanye kazi kwa pamoja kwa kuzingatia umuhimu wa kila mmoja wetu,” alisema Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga aliwakumbusha watumishi hao jukumu lao kuu ambalo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji na aliwataka kuhakikisha wanatekeleza jukumu hilo kwa ufanisi na ubunifu mkubwa ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Alibainisha kwamba endapo kila mtumishi atatimiza majukumu yake kama inavyostahili, huduma itaboreka zaidi na maeneo mengi yatafikiwa hasa ikizingatiwa kwamba Jiji la Mwanza linakuwa kwa kasi.

“Tunapaswa kwenda na kasi ya ukuaji wa Jiji letu, hatupaswi kuachwa nyuma; kadri Jiji linavyozidi kutanuka nasi hatuna budi kutanua huduma zetu na busara zaidi ni kufika mbali zaidi kwa maana yakufika kwenye maeneo ambayo bado Jiji halijafika,” alisema Mhandisi Sanga.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Edith Mudogo aliwaasa watumishi wote kuwa wazalendo na aliwataka watumie nafasi walizonazo kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kama inavyostahili.

Alisema MWAUWASA inawatumishi wa kada mbalimbali na kwamba yampasa kila mtumishi kwa kada yake afikirie namna bora ya kuhakikisha huduma ya maji inaimarika na kuwafikia wananchi wengi zaidi hususan wale wa maeneo ya pembezoni.

“Hapa tuna watumishi wa kada mbalimbali, sasa itapendeza kila mtumishi kwa kada yake atazame ni vipi anaweza kuwa na mchango wa kusambaza huduma hii ya maji kwa wananchi waishio maeneo ya pembezoni,” alisema Mudogo.

Aliwahakikishia ushirikiano kutoka kwa Bodi ya Wakurugenzi hasa ikizingatiwa kwamba dhamira ya Bodi ni kuona wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya maji bila kujali maeneo waliyopo.

“Sisi kama wajumbe wa Bodi matamanio yetu ni kuona wananchi wote wa Jiji la Mwanza wanapata huduma ya maji kutoka MWAUWASA; hatupo tayari kuona mnashindwa kutimiza majukumu yenu, tupo nanyi, tufanye kazi,” alisisitiza.

Aidha, mkutano huo ulitumika kutambua jitihada za watumishi waliofanya kazi MWAUWASA kwa miaka 15 ambapo watumishi sita walikabidhiwa tuzo za utumishi wa muda mrefu ikiwa ni ishara ya kutambua jitihada zao za muda mrefu katika kuwahudumia wananchi.

Tuzo hizo za utumishi wa muda mrefu hutolewa kila mwaka ambapo mtumishi anayetimiza miaka 15 hukabidhiwa ikiwa ni ishara ya kutambua utumishi wake kwa muda wote huo. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527