NDUGAI AWAPONDA KIAINA WABUNGE WANAOMILIKI BODABODA NA NOAH 'UNAMTIA AIBU SPIKA'

Spika  wa Bunge, Job Ndugai, ametoa wito kwa wabunge kuwekeza kwenye sekta ya elimu badala ya magari aina ya Noah au pikipiki, akieleza kuwa wanamtia aibu.

 
Ndugai alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akitangaza wageni wa Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza (CCM), ambao ni wanafunzi waliofanya vizuri kidato cha nne na darasa la saba mwaka 2018.

Wanafunzi waliotambulishwa ni waliomaliza kidato cha nne mwaka 2018 katika Shule ya Sekondari Sunshine na kupata ufaulu wa daraja la kwanza na pili.

"Pia kuna wanafunzi 59 waliomaliza darasa la saba mwaka 2018 kutoka Shule ya Msingi ya Anne Marie Academy ya jijini Dar es Salaam, kwenye wilaya, hii shule ya ilikuwa ya kwanza na kimkoa ilikuwa ya kwanza na kitaifa ilikuwa ya sita," alisema.

Kutokana na ufaulu huyo, Spika Ndugai alimpongeza Rweikiza ambaye ni mmiliki wa Shule ya Anne Marie kwa kuimarisha elimu.

"Haya ndo mambo ambayo wabunge tunatakiwa tufanye, siyo mbunge unamiliki Noah, unamtia aibu Spika, kila siku unaonekana trafiki huko, mbunge unamiliki bodaboda!

"Tuvuke jamani, bodaboda zikikamatwa, unampigia Spika, Spika bodaboda zangu zimekamatwa huku," Ndugai alisema na kuibua vicheko bungeni.

Kiongozi huyo wa Bunge alitoa rai kwa watunga sheria hao kuwekeza kwenye mambo makubwa, akisema wanapaswa "kuvuka kidogo kwenye uwekezaji".


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527