SERIKALI YASEMA BIASHARA YA KUNI NA MKAA NI HALALI,RASMI NA HAINA KIZUIZI KWA MWANANCHI YEYOTE

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma

Serikali imelieleza bunge kuwa biashara ya kuni na mkaa ni halali,rasmi na haina kizuizi  kwa mwananchi yeyote ili  mradi anafuata mwongozo wa uvunaji wa mazao ya misitu wa mwaka 2007 na marekebisho yake ya mwaka 2015.

Hayo yamesemwa Juni 10,2019 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Costantine Kanyasu wakati akijibu swali la mbunge wa viti Maalum Zubeda Sakuru aliyehoji ongezeko la gharama za nishati nchini hasa umeme na gesi zimepelekea kuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya kuni na mkaa je,lini serikali itarasmisha biashara ya mkaa ili kupunguza makali ya maisha.

Akijibu Swali hilo,Mhe.Kanyasu amesema biashara ya kuni na mkaa inafanyika kwa mujibu wa sheria na kanuni za misitu ,pamoja na tangazo la serikali Na.324  la  14/08/2016  na mwongozo wa uvunaji wa mazao ya misitu wa mwaka 2007 uliofanyiwa marekebisho mwaka2015.

Kutokana na hilo,Naibu Waziri Kanyasu amesema biashara ya kuni na mkaa ni rasmi na haina kizuizi chochote kwa mwananchi na kinachotakiwa ni kufuata sheria  na taratibu za biashara za uvunaji  wa mazao ya misitu.

Aidha,Mhe.Kanyasu amezitaja baadhi ya taratibu ambazo zinatakiwa kufuatwa na kuzingatiwa wakati wa kutaka kufanya biashara ya mkaa na kuni ni pamoja na kutenga maeneo ya misitu kwa ajili ya kutengeneza mkaa,kusajiliwa na meneja wa misitu wa wilaya,kutuma maombi ya usajili kwa afisa misitu wa wilaya na kila mfanyabiashara kulipia mrabaha .

Hata hivyo,serikali imehimiza watanzania kuanzisha mashamba ya miti kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na nishati.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527