Picha : WAZIRI WA NISHATI AFANYA ZIARASHINYANGA, AWASHA UMEME VIJIJINI NA KUMUWEKA NDANI MKANDARASI

Waziri wa Nishati nchini Dkt. Medard Kalemani amefanya ziara mkoani Shinyanga kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini (REA),kufuatilia uimara wa umeme pamoja na kuhamasisha wananchi kulipia shilingi 27,000/= ili waunganishiwe umeme kwenye nyumba zao.

Ziara hiyo imefanyika leo Jumatatu Juni 10,2019 katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambapo Waziri Kalemani amezungumza na wananchi wa Mwakitolyo,Lyabukande,Mahembe na kuwasha umeme katika vijiji vya Mishepo,Itwangi na Ibingo ambavyo awali vilirukwa katika mradi wa REA.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo,Dkt. Kalemani alisema serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 36 kwa ajili ya kufikisha umeme vijijini huku akikisitiza kuwa ifikapo Desemba 2019 vijiji vyote viwe vimepata huduma ya umeme.

“Tunataka ifikapo mwezi Desemba kila kijiji kiwe kimepata umeme,mwananchi utatakiwa kulipia shilingi 27,000/= tu,ukishalipa hiyo wewe dai umeme huhitaji kuuliza nguzo ziko wapi,nguzo siyo jukumu lako…wewe subiri kuunganishiwa tu umeme ndani ya siku saba. Tunataka wananchi wapate umeme bila kujali wanaishi kwenye nyumba za namna gani”,alisema Dkt. Kalemani.

“Tunahitaji kuona taasisi zote zikiwemo shule,zahanati,makanisa,misikiti inapata umeme hata kama zipo mbali kiasi gani na ili kupunguza gharama za kuunganisha mfumo wa umeme ndani ya nyumba ‘Wiring’ tunashauri wananchi  mtumie kifaa cha “UMETA”,alisema Dkt. Kalemani.

Hata hivyo Waziri huyo alieleza kutoridhishwa na kasi ndogo ya Wakandarasi wa mradi wa Umeme Vijijini mkoani Shinyanga Kampuni ya Angelique International Limited’ ambapo aliagiza jeshi la polisi kumuweka chini ya ulinzi Meneja wa kampuni hiyo,bwana Dilip Singh na wenzake,Dilip Patra na Ramashakur.

“Mhe. Mkuu wa wilaya naomba uchukue hati ya kusafiria ya Mkandarasi huyu,badala ya kukaa kwenye Site yeye anaishi India,amekuja leo baada ya kusikia nakuja. Nataka awepo Shinyanga mpaka pale atakapomaliza kufanya kazi tuliyompa,tunataka wananchi wapate umeme,nanyi TANESCO hakikisheni mnaweka vituo kwenye vijiji hatutaki wananchi wawafuate mjini”,aliongeza Dkt.Kalemani.

Awali Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Mhe.Azza Hilal na Mbunge wa Jimbo la Solwa,Ahmed Salum walimweleza waziri huyo kuwa mradi wa umeme vijijini umekuwa ukisuasua mkoani Shinyanga kutokana na kasi hafifu ya wakandarasi.

“Mbali na Wakandarasi kuwa wazito katika utekelezaji wa mradi wa REA,changamoto nyingine ni baadhi ya vijiji kurukwa hivyo kwenye baadhi ya vijiji wananchi wamekuwa watazamaji tu wa nyaya na nguzo za umeme,nakuomba Mhe. Waziri uwahurumie wananchi hawa nao wapate umeme”,alisema Mhe. Azza huku amepiga magoti mbele ya Waziri Kalemani.

NIMEKUWEKEA PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA ZIARA YA WAZIRI KALEMANI...Tazama hapa chini
Waziri wa Nishati nchini Dkt. Medard Kalemani (wa pili kulia) akiteta jambo na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe.Jasinta Mboneko wakati akiwasili katika kijiji cha Mahembe kilichopo katika kata ya Mwakitolyo halmashauri ya wilaya ya Shinyanga akiwa katika ziara yake mkoani Shinyanga kukagua utekelezaji wa mradi wa Umeme Vijijini (REA awamu ya tatu).Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Solwa, Mhe. Ahmed Salum.Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Mhe. Ngasa Mboje akifuatiwa na Mbung wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga ,Mhe. Azza Hilal. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Waziri wa Nishati nchini Dkt. Medard Kalemani akiwahamasisha wakazi wa Mahembe kulipia shilingi 27,000/= ili waunganishiwe huduma ya umeme kwenye nyumba zao.
Hapa ni katika kijiji cha Lutolyo zoezi la kuweka nguzo za umeme likiendelea : Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akitoa maelekezo kwa Wakandarasi wa mradi wa Umeme Vijijini kuhakikisha wanatumia wananchi wa kwenye vijiji kama vibarua badala ya kuleta watu wengine nje ya vijiji.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza katika shule ya Sekondari Mishepo kabla ya kuwasha umeme kwenye shule hiyo iliyopo katika kijiji cha Ng'wang'hosha kata ya Nyamalogo halmashauri ya wilaya ya Shinyanga. Dkt.Kalemani aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akitoa maagizo kwa wakandarasi wa Mradi wa Umeme Vijijini (kulia) kuhakikisha wanasambaza kwenye nyumba zote katika shule ya sekondari Mishepo na kuwapatia umeme wananchi wa vitongoji vyote vya kijiji cha cha Ng'wang'hosha kata ya Nyamalogo halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.  
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwakabidhi walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Mishepo kifaa cha umeme 'UMETA'
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani  akikata utepe ikiwa ni ishara ya Uwashaji umeme katika shule ya sekondari Mishepo.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwasha umeme katika shule ya sekondari Mishepo.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwasalimia wakazi wa kijiji cha Ibingo kata ya Samuye Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambapo aliwahamasisha kulipa shilingi 27,000/= ili waunganishiwe huduma ya umeme.
Mbung wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga ,Mhe. Azza Hilal akimshukuru Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani  kwa kuleta umeme kwenye kijiji cha Ibingo ambacho awali kilirukwa kwenye mradi huku akiomba pia vijiji vingine vilivyosahaulika pia vipatiwe umeme badala ya kubaki watazama nguzo za umeme tu.
Mbunge wa Jimbo la Solwa, Mhe. Ahmed Salum akimuomba Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani kuvipatia huduma ya umeme vijiji vingine vilivyorukwa kwenye mradi wa umeme vijijini.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akikata utepe wakati akiwasha umeme katika nyumba ya bwana Hamis Mgalula mkazi wa kijiji cha Ibingo kata ya Samuye halmashauri ya wilaya ya Shinyanga (wa pili kushoto).
Wananchi wakishuhudia umeme ukiwashwa katika familia ya ya bwana Hamis Mgalula
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akitabasamu baada ya kuwasha umeme katika nyumba ya bwana Hamis Mgalula mkazi wa kijiji cha Ibingo kata ya Samuye halmashauri ya wilaya ya Shinyanga (angalia taa hapo juu...mambo safi kabisa kwenye nyumba ya tembe).
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akimpongeza bwana Hamis Mgalula kwa kupata huduma ya umeme na kuwataka wananchi wengine kulipia shilingi 27,000/= tu ili wafurahie maisha kwa kupata umeme haijalishi unaishi kwenye nyumba ya aina gani.
Msafara wa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ukiwasili katika Kijiji cha Mwakitolyo namba 5 katika kata ya Mwakitolyo halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Mhe. Jasinta Mboneko akimkaribisha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwasili katika Kijiji cha Mwakitolyo namba 5 katika kata ya Mwakitolyo halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na kumweleza kuwa miongoni mwa changamoto katika kata hiyo ni umeme.
Mbunge wa Jimbo la Solwa,Mhe. Ahmed Salum akitoa salamu kwa wananchi wa Mwakitolyo
Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Shinyanga,Mhe. Azza Hilal Hamad akitoa salamu kwa wananchi wa Mwakitolyo.
Wakazi wa Mwakitolyo wakiwa kwenye mkutano.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akimpongeza Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Mhe. Azza Hilal na Mbunge wa Jimbo la Solwa, mhe. Ahmed Salum kwa jitihada mbalimbali wanazofanya katika kuwasaidia wananchi ikiwemo kuwapigania kupata huduma ya umeme. 
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwaagiza wataalamu wakiwemo wakandarasi na viongozi wa TANESCO kuhakikisha wanasimika nguzo za umeme haraka iwezekavyo Mwakitolyo ili wananchi waanze kupata huduma ya umeme. Mwakitolyo namba 5 ni miongoni mwa vijiji ambavyo vilikuwa vimerukwa kwenye mradi wa REA.
Wakazi wa Mwakitolyo wakimsikiliza Dkt. Kalemani.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani  akiwahamasisha wananchi kutumia kifaa 'UMETA' ili kupunguza gharama za kuunganisha mfumo wa umeme majumbani.
Wakazi wa Mwakitolyo wakigombania UMETA baada ya kupewa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani. 
Wakazi wa Mwakitolyo wakifuatilia matukio yaliyokuwa yanaendelea.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akimsikiliza mmoja wa wazee wa kijiji cha Mwakitolyo namba 5.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwahamasisha wakazi wa Kijiji cha Lyabukande kata ya Lyabukande kulipia shilingi 27,000/= ili wapate huduma ya umeme.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akisalimiana na wazee wa kijiji cha Itwangi kata ya Itwangi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga baada ya kuwasili tayari kwa kuwasha umeme katika kijiji hicho.
Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Shinyanga,Mhe. Azza Hilal akisalimiana na Waswezi waliokuwa wanatoa burudani wakati Waziri wa Nishati,Dkt.Medard Kalemani akiwasili katika kijiji cha Itwangi.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akipiga makofi baada ya kukata utepe ishara ya kuwasha umeme katika shule ya msingi Luhumbo iliyojengwa mwaka 1945.
Viongozi mbalimbali wakifurahia baada ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani kuwasha umeme katika shule ya msingi Luhumbo iliyopo katika kijiji cha Itwangi.
Diwani wa kata ya Itwangi Jilala Sonya akizungumza katika mkutano katika kijiji cha Itwangi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Mhe. Jasinta Mboneko akimkaribisha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani katika kijiji cha Itwangi.
Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Shinyanga,Mhe. Azza Hilal akipiga magoti kumuomba Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani vijiji ambavyo havina huduma ya umeme ikiwemo Danduhu,Chembeli,Bukumbi,Mwamkanga,Mwanono,Nyambui,Usule n.k vipatiwe huduma ya umeme badala ya kubaki kuwa watazamaji wa nguzo za umeme.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akisalimiana na wakazi wa kijiji cha Itwangi.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiagiza wakandarasi wa mradi umeme vijijini kutoka Kampuni ya Angelique International Limited’ kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa kushindwa kutekeleza kwa wakati kazi ya kuwapelekea umeme wananchi. Wa tatu kushoto ni Meneja wa kampuni hiyo,bwana Dilip Singh na wenzake wawili raia wa India ,Dilip Patra na Ramashakur (kulia).
Askari polisi wakimpeleka kwenye gari la polisi Meneja wa Kampuni ya Angelique International Limited’,bwana Dilip Singh na wenzake wawiliDilip Patra na Ramashakur.
Meneja wa Kampuni ya Angelique International Limited’  ,bwana Dilip Singh na wenzake wawiliDilip Patra na Ramashakur wakipanda kwenye gari la polisi.
Meneja wa Kampuni ya Angelique International Limited’  ,bwana Dilip Singh na wenzake Dilip Patra na Ramashakur wakiwa ndani ya gari la polisi.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akihamasisha wananchi kutumia UMETA.
Baada ya kumaliza ziara : Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akitoa maelekezo kwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Mhe. Jasinta Mboneko (katikati) kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga na Meneja wa TANESCO mkoa wa Shinyanga,Mhandisi  Fedgrace Shuma (kulia).
Awali Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga, Mhe. Albert Msovela akitoa taarifa ya mkoa wa Shinyanga kwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Awali Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Shinyanga,Mhe. Azza Hilal Hamad akimweleza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani  changamoto ya kasi ya wakandarasi wa umeme vijijini na tatizo la baadhi ya vijiji kurukwa kwenye mradi wa REA.
Awali Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akielezea lengo la ziara yake mkoani Shinyanga. 
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527