SADIO MANE KUWAKOSA TAIFA STARS



Mkufunzi wa Senegal Aliou Cisse amethibitisha kuwa nyota wake wa Liverpool Sadio mane amepigwa marufuku ya mechi moja hivyobasi hatoshiriki katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Taifa Stars ya Tanzania nchini Misri.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 atakosa mechi ya kundi C dhidi ya Tanzania tarehe 23 mwezi Juni mjini Cairo baada ya kupewa kadi mbili za njano katika mechi ya kufuzu ya Senegal.

''Kutokuwpo kwake hakutatuathiri kwa njia yoyote'' , kocha Cisse aliambia vyombo vya habari vya Senegal kabla ya kuondoka katika kambi yao ya mazoezi katika eneo la Alicante Uhispania kuelekea Misri.

''Ni kweli kwamba uwepo wake ni muhimu sana kwetu lakini bila yeye tuko dhabiti.Shirikisho la soka CAF limeamua hivyobasi hatuna budi'', Cisse aliongezea.



Sadio Mane ameichezea Senegal mara  60 na kuifungia magoli 16

Mane alipewa kadi ya njano katika mechi ambayo Senegal ilipata ushindi wa 1-0 dhidi ya Equitorial Guinea mnamo tarehe 17 Mwezi Novemba 2018 na pia alipokea kadi nyengine ya njano katika mechi ya ushindi wa 2-0 dhidi Madagascar mnamo tarehe 23 mwezi Machi 2019 ijapokuwa haijathibitishwa katika takwimu za mechi za Caf.


Mchuano huo nchini Misri, unaotarajiwa kuanza tarehe 21 mwezi Juni hadi 19 Julai , utakua wa Mane wa nne wa Afcon na itakuwa mara ya pili kukosa mechi ya ufunguzi ya Senegal.

Alikosa mechi ya ufunguzi ya Simba hao wa Teranga katika fainali za 2015 nchini Equitorial Guinea dhidi ya Ghana kwa kuwa alikuwa anauguza jeraha la kifundo cha mguu alilopata alipokuwa akiichezea klabu yake ya zamani Southampton.

Mane , ambaye alishinda taji la ligi ya mabingwa Ulaya akiichezea Liverpool mwezi huu, alijiunga na Simba wa Teranga katika mazoezi nchini Uhispania siku ya Alhamisi kabla ya yeye na wenzake kuelekea Misri siku ya Ijumaa.

Anatarajiwa kucheza mechi nyengine za Senegal mjini Cairo dhidi ya Algeria tarehe 27 mwezi Juni na Kenya siku nne baadaye.

CHANZO.BBC SWAHILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527