RAIS MSTAAFU MKAPA AKUMBUKA ALIKOSOMA


Katika kuonesha anathamini alikotoka kielimu, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa anatarajiwa kuungana na wahitimu wengine wa shule kongwe ya Sekondari Ndanda ya Masasi, Mtwara kuitembelea shule yao Septemba 27, mwaka huu kwa ajili ya Siku ya Wahitimu wa shule hiyo iliyoanzishwa miaka 91 iliyopita.

Mkapa aliyesoma Ndanda katika miaka ya 1950, alithibitisha kuungana na wahitimu wengine wa shule hiyo alipokutana na kuzungumza na viongozi wa Umoja wa Wahitimu wa Shule ya Sekondari Ndanda (UWAHISSENDA) waliokwenda kuutambulisha umoja wao ofisini  kwake jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Alisema, kama mmoja wa waliobahatika kusoma Ndanda, anajiona ana wajibu wa kuungana na wana umoja wengine walioanzisha wazo la kuitembelea shule yao ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa shule katika maisha yao.

“Hili ni wazo la kupongezwa sana. Hongereni kwa ubunifu na uthubutu wa kutambua umuhimu wa kule mlikopata elimu. Ni wachache sana wanaokumbuka mambo kama haya,” alisema Mkapa huku akiahidi mwaka huu ataungana nao.

Kwa wahitimu hao, hii Hii itakuwa mara ya pili kurejea Ndanda, kwani mwaka jana walikwenda kwa mara ya kwanza na kuzindua umoja wao wakiwa shuleni hapo na kukabidhi vitabu vyenye thamani ya takribani Sh milioni 5, kupanda miti, kuzungumza na wanafunzi wa sasa na pia kushiriki katika shughuli mbalimbali shuleni hapo, ikiwa ni pamoja na kufyatua matofali.

Mwenyekiti wa umoja huo, Yohana Kasawala alimshukuru Rais Mstaafu kwa kuridhia kuwa mwanachama mpya, lakini kipekee kwa kukubali kuungana na wanafunzi wengine wa zamani kwa safari ya shuleni Ndanda. Aliwataka wahitimu wengine kuona fahari ya kusoma Ndanda na hivyo wajitokeze kufanikisha Siku ya Wahitimu Ndanda.

Umoja huo uliasisiwa mwaka 2015 kupitia mtandao wa kijamii wa Whatsapp na tayari una wanachama hao zaidi ya 150, wakiwa na malengo ya kutanua wigo wa ukaribu hata baada ya kuhitimu masomo yao, kuinuana kiuchumi na pia kushiriki katika kuijengea uwezo shule yao.

 “Daima umoja ni nguvu, utengano ni dhaifu, nasi tumeona ni vyema tukatumia mshikamano huu kama fursa ya kujiimarisha kiuchumi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527