NAIBU KAMISHNA MKUU TRA ATEMBELEA BANDARI KAVU ZA ICD


Na Veronica Kazimoto
Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Msafiri Mbibo ametembelea bandari kavu ya Said Bakhresa (SSB-ICD) na African ICD ambapo amewataka Maofisa Forodha wa Mamlaka hiyo kuzingatia uwajibikaji, weledi na uadilifu wakati wote wanapotimiza majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza na maofisa hao kabla ya kukagua mizigo iliyopo katika bandari hizo, Naibu Kamishna Mkuu huyo amesema kwamba, uzingatiaji wa maadili katika sehemu za kazi utasaidia kuondoa malalamiko na kero kwa walipakodi ambao ni wadau wakuu wa TRA.

“Jukumu la kujenga taswira ya mamlaka ni la kila mtumishi wa TRA. Hivyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anafanya kazi bila upendeleo, anawajali wateja ikiwa ni pamoja na kutumia lugha yenye staha, alisema Naibu Kaimshna Mkuu Mbibo.

Kwa upande wake Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Ben Usaje amewasisitiza watumishi hao kutojihusisha na vitendo vya rushwa ambavyo vinaichafua Mamlaka ya Mapato Tanzania.

“Sote humu ndani tunajua kuwa, kupokea au kutoa rushwa ni kinyume cha sheria ya nchi yetu na yeyote atakayebainika akifanya hivyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Hivyo, hakikisheni mnaepuka kabisa vitendo hivyo vya rushwa kwani vitawasababishia kupoteza kazi na kufikishwa mahakamani”, alisema Usaje.

Baadhi ya majukumu ya Ofisi za Forodha zilizopo katika bandari kavu hapa nchini ni kuhakikisha kuwa taratibu zote za kuingiza mizigo ndani ya nchi zinafuatwa pamoja na kuhakikisha kwamba kodi stahiki inalipwa na wenye mizigo kabla ya kutoa mizigo yao katika bandari hizo.

MWISHO.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527