WMU – Arusha
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla amepongeza juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali kutangaza utalii na uanzishwaji wa kampeni zinazohamasisha mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kupitia vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.
Dkt. Kigwangalla ametoa pongezi hizo leo mkoani Kilimanjaro wakati wa hafla fupi ya kuwaaga Wapanda mlima 32 na Waendesha Baskeli 28 kutoka nchi mbalimbali walioshiriki kupanda mlima Kilimanjaro kupitia Kampeni ya Geita Gold Mining Kilimanjaro Challenge 2019 inayolenga kukusanya fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi na kuwasaidia watoto yatima.
Amesema kampeni hiyo itawawezesha wapanda mlima hao kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro (Uhuru Peak) na waendesha Baiskeli kuzunguka mlima Kilimanjaro takribani Kilometa 500 ikiwa ni sehemu ya kushiriki katika changamoto ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika mwitikio dhidi ya VVU na Ukimwi.
“Ugonjwa wa UKIMWI umeendelea kuwa suala la kipaumbele kwa Serikali, athari zake zinagusa sekta zote ikiwemo wizara ninayoiongoza ya Maliasili na Utalii, bila shaka sote tumeona jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa kupambana na janga hili” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla
Amesema kuwa pamoja na takwimu kuonesha kupungua kwa maambukizo mapya bado jitihada zaidi zinahitajika ili kuutokomeza ugonjwa huo akifafanua kwamba kila mwananchi ni lazima awe macho kuhakikisha anashiriki kutokomeza ongezeko la maambukizo mapya.
Aidha, amefafanua kuwa programu hiyo imetoa mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Mlima Kilimanjaro wakati na baada ya msimu wa Kill Challenge kumalizika kwani wageni kutoka ndani nan je ya Tanzania huwataarifu wenzao pindi wanaporudi makwao ili waweze kuja kupanda mlima Kilimanjaro.
“Huu ni uthibitisho tosha kwamba programu hii siyo tu inachangia kudhibiti Ukimwi bali pia inachangia kukuza uchumi wa nchi yetu kupitia mapato ya utalii ya Mlima Kilimanjaro” Amesema.
Dkt. Kigwangalla ameipongeza kampuni ya GGL na wawekezaji wote ambao wamekua wakijitoa kuchangia ustawi wa jamii ya watanzania akitoa wito kwa makampuni mengine kuendelea kujitolea kuchangia program hiyo pamoja na Mfuko wa hisani wa UKIMWI ulioanzishwa na Serikali wa AIDS Trust Fund (ATF).
Amesema hatua ya GGL kushirikiana na Serikali kupitia TACAIDS ni ya kupigiwa mfano na kwamba inaonesha namna sekta binafsi hususani wafanyabiashara wanavyoendelea kujitokeza kuchangia mwaka hadi mwaka.
Ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa program hiyo takribani shilingi bilioni 13 za Kitanzania zimekusanywa kupitia jitihada hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko amewapongeza wadau wote kwa kuendelea kuchangia kwenye Mfuko wa kupambana na Ukimwi.
Amesema kuwa mujibu wa takwimu zilizopo TACAIDS ugonjwa wa UKIMWI bado ni tatizo nchini kutokana na kuwepo kwa maambukizi mapya ya watu 200 kila siku.
Amesema kazi kubwa inayofanywa na TACAIDS kwa sasa ni kuendeleza kampeni ya kuzuia maambukizi yasitokee ili kuendana na makubaliano ya umoja wa Mataifa ya kufikia maambukizo 0 ifikapo mwaka 2030.
“ Bado tunayo kazi kubwa sana ya kuzuia maambukizi haya, watu 200 kwa siku kuambukizwa VVU ni wengi, tunaendelea kujitahidi na kufanya kazi kubwa ya kuelimisha wananchi na kama ingekua ni ajali ingekua ni watu 200 wanaumia kila siku, tunazungumza hizi takwimu kujikumbusha kwamba Ukimwi bado upo” Amesisitiza Dkt. Maboko.
Ameeleza kuwa kiwango cha maambukizi hayo kinazidi kuongezeka miongoni mwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 akifafanua kwamba kwamba kati ya watu 200 waliopata maambukizi , watu 80 ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24.
“ Kwa ujumla maambukizi mapya yanazidi kushuka isipokuwa kwa vijana yanazidi kupanda juu, sisi kama Tume kwa kushirikiana na wadau tunaliona na tunaendelea kulifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kunusuru kizazi cha vijana ambao ndilo tegemeo la Taifa na viongozi wa baadae” Amesisitiza Dk. Maboko.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI Mhe. Oscar Mukasa amesema kuwa kazi yao kama Kamati ni kushirikiana na wadau wote katika masuala ya Sera, Sheria na usimamizi na kufafanua kuwa mfuko wa Ukimwi tangu kuanzishwa kwake umekuwa na changamoto ya kupata fedha akiupongeza Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa kuendelea kuchangia fedha katika mfuko huo.
Amesema Bunge itaendelea kuishauri Serikali kwa lengo la kupata vyanzo vingine vya mapato vya uhakika ili Serikali iweze kushirikiana na wadau wa ndani wa Sekta binafsi kwa lengo la kujitegemea.
Amesema tukio hilo la wapanda mlima kuchangisha fedha linapeleka ujumbe kwa jamii kwamba kazi ya kupambana na UKIMWI bado ni kubwa na endelevu hivyo jamii yote inapswa kushiriki kikamilifu.
MWISHO.