MKANDARASI WA MRADI WA UMEME WA RUFIJI (MW 2115) KUANZA UJENZI RASMI LEO JUNI 15, 2019.


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (watatu kushoto), akiwa na Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, (wapili kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Tito Mwinuka (wapili kulia) wakiwa site (eneo la ujenzi wa mradi wa umeme wa maji mto Rufiji) mapema leo Juni 15, 2019.

Imeelezwa kuwa, Mkandarasi wa mradi wa umeme wa Rufiji, kampuni ya JV Arab Contractors na Elsewedy Electric anaanza rasmi kazi za ujenzi wa mradi huo leo tarehe 15/6/2019.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani baada ya ziara ya kukagua kazi za maandalizi ya awali ya ujenzi wa mradi huo akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka na watendaji wengine kutoka Kampuni ya Mkandarasi, Wizara ya Nishati na  TANESCO.

Mkandarasi huyo anaanza ujenzi ikiwa ni baada ya kufanya matayarisho mbalimbali  ikiwemo upelekaji wa vifaa vitakavyotumika katika shughuli za ujenzi, uwepo wa kambi za Wafanyakazi, Ofisi na kukamilisha kazi nyingine za awali ambapo kwa mujibu wa mkataba.

Alipewa miezi Sita ya kufanya kazi hizo ambayo ukomo wake ulikuwa Juni 14, 2019.

Dkt Kalemani alisema kuwa, kazi anazoanza nazo leo ni upasuaji wa miamba ili kuruhusu maji kupita  kwenda kwenye mitambo ya kufua umeme.

Alisema kazi nyingine za awali zitakazofanywa ni kujenga daraja la muda litakaloruhusu upitishaji wa vifaa kwenda kwenye eneo jingine la kazi pamoja na ujenzi wa daraja la kudumu.

Dkt Kalemani alieleza kuwa, Mkandarasi ameahidi kukamilisha mradi huo ifikapo mwezi Juni, mwaka 2022 na mradi utatekelezwa kwa kasi na ikiwezekana, megawati zote 2115 zitapatikana kwa wakati mmoja.

Kuhusu vifaa vitakavyotumika kwenye mradi huo, Dkt Kalemani aliwataka kutumia vifaa vinavyopatikana nchini na kwa vifaa visivyopatikana nchini, vitanunuliwa baada ya kupata kibali maalum.

Pia aliagiza Wataalam wa ndani kupewa kipaumbele katika ujenzi wa mradi huo, ili waweze kusimamia mradi huo mara baada ya mkandarasi kukamilisha kazi.

Aidha, aliwapongeza TANESCO na TANROADS kwa kusimamia mradi huo ipasavyo, na kuwaagiza kuendelea kuwasimamia wakandarasi usiku na mchana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post