DC MBONEKO AFANYA ZIARA KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI KIJIJI CHA BUCHAMA - TINDE.... SANGOMA ATUHUMIWA KUUA WANAWAKEMkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko, amefanya ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika kijiji cha Buchama kata ya Tinde halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, na kuwataka wananchi wajitume kufanya kazi pamoja na kuchangia shughuli za maendeleo sambamba na kudumisha amani na utulivu.

Mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi wa kijiji cha Buchama umefanyika leo Juni 21, 2019 katika kitongoji cha Saku Sentani na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya wananchi wa kijiji hicho, ambapo walitoa kero zao kwa mkuu huyo wa wilaya.

Awali wananchi wakiwasilisha matatizo yao kwa mkuu wa wilaya,Mhe. Jasinta Mboneko kero yao kubwa ilikuwa ni kuomba ulinzi na usalama uimarishwe katika kijiji hicho, ambapo kumeanza kutokea matukio ya mauaji ya wanawake kwa kukatwa mapanga na kisha kutolewa viungo vyao vya mwili.

Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Maganga Mhamila, amesema maisha yao yapo hatarini hasa wanawake ambao ndiyo wamekuwa wakiwindwa kuuawa kwa ajili ya kutolewa viungo vyao zikiwemo sehemu za siri, kitendo ambacho kimewanyima amani na kushindwa kufanya hata shughuli za kiuchumi.

“Mkuu wa wilaya kwenye kijiji hiki kuna mganga mmoja amekuwa akiagua kwa kupiga ramli chonganishi na kusababisha mauaji, ambapo hivi karibu kuna mwanamke aliuawa porini kwa kuchinjwa na kisha kutolewa viungo vyake yakiwemo matiti, masikio na sehemu za siri ,”amesema Mhamila.

“Lakini tulitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji na hatua zaidi zikachukuliwa na polisi wakamchukua mganga huyo, cha kushanghaza ndani ya siku mbili tukamuona hapa kijijini na kuanza kutamba kuwa mwenye hela hawezi kufanywa jambo lolote na kuendelea kutishia watu hasa wale ambao walitoa taarifa zake, kuwa atawaua kwa mapanga au kuwaroga,”ameongeza.


Naye mwenyekiti wa kijiji hicho Rahel Kinga, alikiri kuwepo kwa tukio la mwanamke kuuawa kwa kukatwa mapanga, na kubainisha kuwa hatua ambazo walizichukua ni kuwasiliana na jeshi la polisi, ambalo nalo limeonekana kushindwa kazi kutokana na mtuhumiwa kumwachia huru, na hivyo kumuomba mkuu huyo wa wilaya aje awasaidie kumaliza tatizo hilo.

Kufuatia malalamiko hayo, mkuu huyo wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Shinyanga, ameliagiza Jeshi la Polisi kumkamata mganga huyo popote pale alipo pamoja na wafuasi wake ili uchunguzi uanze mara moja juu ya tuhuma hizo.

Pia aliwataka wananchi wa kijiji hicho washirikiane kikamilifu na vyombo hivyo vya dola, kwa kutoa ushahidi wa kutosha juu ya tuhuma hizo za mganga kuhusika na mauaji ya wanawake kwa kuwakata mapanga, ili apate kuchukuliwa hatua kali za kisheria na kijiji kibaki kuwa salama na amani na utulivu.

Katika hatua nyingine alitoa wito kwa wananchi wa kijiji hicho kujituma kufanya kazi pamoja na kuchangia shughuli za maendeleo, huku kero zao walizozitaja serikali itazifanyia kazi, ikiwamo kuwaletea mradi wa maji safi na salama, kuwajengea mtaro wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara.

Na Marco Maduhu - Malunde1 blog Shinyanga.

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko, akiwataka wananchi wa kijiji cha Buchama kata ya Tinde Shinyanga vijijini kutoa kero zao zote ili apate kuzipatia ufumbuzi leo kwenye mkutano wa hadhara. Picha zote na Marco Maduhu -Malunde1 blog


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko akitoa majibu ya wananchi juu ya kero zao na kuahidi serikali itazifanyia kazi, huku akiwataka wananchi wakatoe ushahidi juu ya tuhuma za mganga wa kienyeji kuhusika na mauaji ya wanawake kwa kuwakata mapanga, ili apate kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko, akiendelea kuwasisitiza wananchi, kuwa pale maofisa wa polisi watakapo kuja kuchunguza tukio hilo watoe ushahidi na siyo kukimbia , ili mtuhumiwa apate kukutwa na hatia na kufungwa jela tofauti na hapo kazi itakuwa ngumu na kuendelea kulalamikiwa mtuhumiwa kwa nini anaachiwa huru, sababu ya kushindwa kutoa ushahidi.

Mkuu wa wilaya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko pia akiwataka wananchi kujituma kufanya kazi pamoja na kuchangia shughuli za maendeleo na kuwapuuza wale ambao wamekuwa wakikwamisha shughuli hizo hasa wale ma Bush Lawyer ikiwa maendeleo yan letwa na wao wenyewe wananchi.


Wananchi wa kijiji cha Buchama Kata ya Tinde wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wakisikiliza utatuzi wa kero zao kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko, ikiwemo kuwapatia maji safi na salama, pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

Mwenyekiti wa kijiji cha Buchama kata ya Tinde Rahel Kinga, akifungua mkutano wa hadhara wa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, na kuwataka wawe watulivu pamoja na kuwasilisha kero zao ilizipate kukatuliwa.

Mtendaji wa kijiji cha Buchama Tabu Mabula Lugola, akitoa taarifa ya kijiji hicho na kuelezea kero kubwa ni kuanza kutokea kwa matukio ya wanawake kuuawa kwa kukatwa mapanga na kutolewa viungo vyao vya siri.

Mwananchi wa kijiji cha Buchama Maganga Mhamila, akielezea kero kubwa ambayo inawanyima amani kwenye kijiji hicho ni kuanza kuibua kwa matukio ya mauaji ya wanawake kwa kukatwa mapanga na kutolewa viungo vyao vya mwili, zikiwamo sehemu za siri.

Masanja Moto Mgati naye akielezea kwa masikito juu ya matukio ya wanawake kuanza kuuawa kwa kukatwa mapanga hali ambayo inawafanya kukosa amani na kusababisha watu kushindwa kufanya shughuli za kimaendeleo.

Boniphace Mateo akielezea namna alivyoshuhudia maiti ya mwanamke aliyeuawa kwa kuchinjwa na kutolewa viungo vyake vya siri wakati akichunga mifugo porini na kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji.

Diwani wa kata ya Tinde Jafari Kanolo, akielezea kuhusu tukio hilo la muaji ya mwanake kuuawa kwa kukatwa mapanga namna lilivyomnyima usingizi na kuamua kuomba msaada kwa mkuu wa wilaya ili apate kumsaidia kulitatua tatizo hilo na kijiji kibaki kuwa na amani.

Machibya Dotto akitoa kero ya kutojengewa mtaro wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika kijiji hicho ambapo walisha changa hadi kiasi cha shilingi Milioni 3 fedha za nguvu za wananchi lakini hadi leo hajapata msaada wowote licha ya kupewa ahadi mara nyingi.

Charles Kashinje akitoa kero ya ubovu wa barabara, pamoja na kulalamikia maofisa kilimo kutofika kwenye maeneo hayo ili kutoa ushauri wa kilimo bora pamoja na kuwashauri kulima mazao ambayo yanaendana na hali ya hewa ili waweze kupata mavuno mengi na kuinuka kiuchumi.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko, akiwataka wananchi wa kijiji hicho kuwa na utulivu ili waweze kupata majibu ya ufumbuzi wa kero zao, na kumuita Afisa kilimo wa halmashauri hiyo Edward Maduhu atoe majibu yanayohusu masuala ya kilimo.

Afisa kilimo wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Edward Maduhu, akiwatoa hofu wananchi hao kuwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka (2019-20) kuna fedha zimeshatengwa kwa ajili ya kujengwa kwa mtaro huo wa maji ili kufanikisha kilimo hicho cha umwagiliaji.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akimtaka Afisa kilimo wa Kata ya Tinde Hajra Omari kuwa anatembelea wakulima kwa ajili ya kutoa elimu ya kilimo cha kisasa ili wapate mavuno mengi na kuinuka kiuchumi.

Wananchi wa kijiji cha Buchama Kata ya Tinde wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wakisikiliza utatuzi wa kero zao kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko, ikiwamo kuwapatia huduma ya umeme wa REA.

Wananchi wa kijiji cha Buchama Kata ya Tinde wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wakisikiliza utatuzi wa kero zao kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko, ikiwemo ya ukosefu wa minara ya simu ambapo ameahidi kwenda kuongea na makampuni ya simu ili kupeleka minara sehemu hiyo ili waweze kupata mawasiliano mazuri.

Wananchi wa kijiji cha Buchama Kata ya Tinde wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wakisikiliza utatuzi wa kero zao kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko.

Wananchi wa kijiji cha Buchama Kata ya Tinde wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wakisikiliza utatuzi wa kero zao kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko.

Awali katibu tawala wa wilaya ya Shinyanga Boniphace Chambi akiwasalimu wananchi wa kijiji cha Buchama Kata ya Tinde na kuwataka watumie fursa ya kutoa kero zao ikiwa mkuu wao wa wilaya amewatembelea ili kutatua kero zao.

Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post