AUA MKE WAKE KISHA NAYE KUJIUA KWA KUJITEKETEZA KWA MOTO

Watu wanne wamefariki dunia katika matukio matatu tofauti likiwamo la mwanaume kumuua mpenzi wake kisha naye kujiua kwa kujiteketeza na moto kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi.

Taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari Jumatano, Juni 19, 2019 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro ilisema tukio hilo limetokea juzi Jumanne Juni 18, 2019, Saa 10:00 jioni mtaa wa Mhandu kisiwani jijini Mwanza na kuwataja marehemu kuwa ni Fungo Mayala (34) na Hamida Joseph (30)

Kamanda Muliro amesema tukio hilo limesababishwa na mgogoro wa kimapenzi wa muda mrefu na mwanamke aliwahi kuripoti tukio hilo kituo cha polisi na mtuhumiwa alikamatwa na kufikishwa mahakamani Juni 16, 2019.

Kwa mujibu wa Muliro, kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa Juni 18 na Hamida alienda mahakamani kuomba Mahakama iridhie kumsamehe mshtakiwa huyo na kuondoa kesi mahakamani hapo.

“Baada ya msamaha huo, mtuhumiwa alienda nyumbani kwa marehemu na kuingia ndani kisha alifunga mlango na kuanza kumpiga, majirani walisikia kelele za Hamida akiomba , ndipo walitoa taarifa kituo cha polisi waliofika na kukuta nyumba yote inafuka moshi,” amesema Muliro.

Kamanda huyo amesema polisi walishirikiana na majirani kuvunja mlango na walipofanikiwa walimkuta Hamida keshafariki dunia na alikuwa ameungua moto sehemu mbalimbali za mwili wake huku mtuhumiwa akikutwa mahututi na alifariki njiani wakati wanampeleka hospitali.

Katika tukio lingine, mtu mmoja Shiganga Luheke (38) mkazi wa Mtale ameuawa na kundi la watu wenye hasira baada ya kukamatwa na kuku wawili wa wizi katika kijiji cha Itandula.


Tukio hilo limetokea Juni 17 saa sita usiku akiwa na kuku hao aliodaiwa kuwaiba ndipo walimshambulia kwa kumpiga kwa mawe na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kusababisha mauti yake.

Katika tukio hilo, polisi wanamshikilia mwenyekiti wa kitongoji hicho kutokana na kuhusiska kwa namna moja ama nyingine katika mauaji hayo.

Katika tukio la tatu, mtu mmoja, Joshua Monge (40) mganga Mkuu wa wilaya ya Ukerewe amefariki dunia baada ya gari alilokuwa akiendesha aina ya Toyota Ipsum kumgonga mtembea kwa miguu, Athuman Nandoya (45) mkazi wa Nyamanoro kisha kuingia mtaroni.

Ajali hiyo imetokea Juni 16, saa 11 alfajiri ambapo majeruhi amekimbizwa hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou-Toure kupatiwa matibabu huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa hapo pia.
Na Ngollo John - Mwanza

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post