MAALIM SEIF ATEULIWA KUWA MSHAURI MKUU WA CHAMA CHA ACT- WAZALENDO


Kamati Kuu ya Chama ACT wazalendo kimemteua aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad kuwa Mshauri Mkuu wa chama hicho, ikiwa ni miezi michache tangu atangaze kujiunga na chama hicho.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Juni 10, 2019 na Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi, Ado Shaibu, kufuatia kikao cha kamati kuu ya ACT Wazalendo kilichoketi Dar es Salaam jana Jumapili, imesema Maalim Seif mwenye kadi namba moja ya chama hicho, ameteuliwa kuwa mshauri mkuu wa chama.

Katika nafasi za kamati kuu ya chama hicho, wafuasi wa Maalim Seif wameingizwa akiwemo Fatma Fereji na Eddy Riyami, huku pia kukiwa na wajumbe wengine waliongezwa ambao ni Theopista Kumwenda na Mwajabu Dhahabu.

Katika nafasi za wenyeviti wa Kamati za Kitaifa, Nassor Marzurui ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Miradi, huku Salim Bimani akiteuliwa kuwa  Mwenyekiti wa Kamati ya Itikadi, Mawasiliano na Uenezi na Joram Bashange akiteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya kampeni na uchaguzi.

Wengine ni pamoja na Ismail Jussa aliyeteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya mikakati, usimamizi na ufuatiliaji, huku mbunge wa zamani wa viti maalum. Mhonga Ruhwanya akiteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya oganaizesheni, mafunzo na wanachama.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527