MAGHUBA YA TAKA YAHATARISHA AFYA ZA WATOTO MBEYA


Mmoja wa watoto jijini Mbeya akichezea taka katika ghuba la kukusanyia taka lililopo jirani na shule ya msingi Sinde jijini hapo.Watoto kucheza maeneo yenye taka kama haya inatajwa kuhatarisha afya zao.(Picha na Joachim Nyambo)

Watoto waishio jirani na maeneo yaliyotengwa kwaajili ya kukusanyia taka katika maeneo mbalimbali jijini Mbeya wametajwa kuwa hatarini kupata magonjwa ya Mlipuko ikiwemo Kipindupindu na kuhara kutokana na watoto hao kucheza katika maeneo yasiyo safi na salama.

Uchelewaji wa uzoaji taka kwenye maeneo hayo kabla ya kuzipeleka kwenye Dampo maalumu la jiji lililopo Nsalaga jijini hapo umetajwa kuchangia zaidi athari kwa watoto hao kwakuwa wapo baadhi yao ambao hudhubutu kwenda kuchambua mabaki ya vyakula kama miwa na matunda kwenye taka hizo na kula pasipokujua athari inayoweza kuwakumba.

Kufuatia hali hiyo wakazi waishio au kufanya shughuli zao hususani za kibiashara jirani na maeneo ya kukusanyia taka wamepaza sauti wakisema wamechoshwa na uhatarishaji Afya za watoto wao na kuzitaka mamlaka husika kuchukua hatua ili kuwanusuru pia na gharama za matibabu.

Daines Mwatobolo ni kikongwe wa miaka 70 anayeishi na wajukuu sita na vitukuu sita ambapo katika mahojiano alisema familia yake ni miongoni mwa zile zilizoathirika kiafya kutokana na uwepo wa ghuba la kuhifadhia taka lililopo nje ya nyumba yake mtaa wa Ilolo,kata ya Isanga jijini Mbeya.

Kikongwe huyo alisema Ghuba hilo limekuwa kero kubwa kwake na wanafamilia kwakuwa taka zinazotupwa ikiwemo mizoga ya wanyama huoza na kuleta harufu kali ambayo huingia hadi ndani ya vyumba wanavyolala na kuwasababishia adha kubwa na magonjwa kama mafua na vikohozi.

Alisema wajukuu zake pia mara kadhaa wameugua magonjwa ya kuhara hatua anayoaamini inatokana na wao na wenzao majirani kuchezea taka kwenye ghuba hilo ambapo mara kadhaa amekuwa akifanya juhudi za kuwakanya lakini kuna wakati anashindwa.

“Kinachotushangaza zaidi ni pale wanapotuambia ukiugua kipindupindu ukitibiwa ukapona itabidi ushitakiwe utozwe faini…tunajiuliza hivi wao ndiyo wametuletea hizi taaka mlangoni..tunateseka nazo..zinahatarisha maisha yetu halafu wanataka kututoza faini!Hii si sawa tunaomba wazinusuru familia zetu,tunaumia sana,watoto wanapata shida wapi wakacheze.”alisema.

Mkazi mwingine wa mtaa huo,Benson Japhet aliitaja changamoto ya kutozolewa kwa wakati taka zinazokusanywa hapo kuchangia zaidi kuhatarisha afya za watoto wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi zilizopo jirani ikiwemo Wigamba,Sinde na Isanga ambao hupita hapo na kuokota mabaki ya vyakula hasa miwa.

Afisa Afya Hospitali ya Mkoa wa Mbeya Musa Juma alisema zipo athari nyingi kwa watoto kucheza kwenye maeneo yenye taka ukiachilia mbali kujeruhiwa na vitu vyenye ncha kali vinavyokusanywa pamoja na takataka kwenye maeneo husika.

Alisema magonjwa ya aina mbalimbali yanaweza kuambukizwa kwa watoto na ndiyo sababu wwatu wote wanaofanya shughuli zinazohusiana na uzoaji taka hupewa chanjo na kinga za aina mbalimbali ili kuzuia maambukizi ya magonjwa.

“Kwa mazingira ya watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi kutokana na uwepo wa mlundikano wa taka zipo athari nyingi kwao zinaweza kujitokeza kiafya.Wanaweza kucheza katika mazingira hayo pasipo kujua athari zilizopo hasa kutokana na umri wao.Na ndiyo maana hata wafanyakazi wanaofanya kazi kitengo cha taka wao wanapata chanjo.Sasa kwa hawa watoto kuna hatari kubwa.” Alisema.

“Kinachotakiwa kufanyika ni jamii kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki ya kuchezea watoto.Taka zihifadhiwe kwenye sehemu stahiki zitakazowaepusha watoto kutozifikia.Na wakati mwingine pia tuepuke kuwatuma watoto kwenda kutupa taka kwakuwa kwa umri wao huwezi jua wanaweza vutiwa na nini kwenye majalala au maghuba na wakaanza kuchezea vitu hivyo pasipo kujua athari ya baadaye.”

Halmashauri ya jiji la Mbeya kupitia Afisa Habari,John Kilia ilibainisha kuwa jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika kuondoa taka kwenye maeneo zinakokusanywa licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali pia zinazokwamisha au kuchelewesha shughuli hizo.

Hivi karibuni akiwa ziarani na wajumbe wengine wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mbeya mjini,Affrey Nsomba alisema kukithiri kwa taka kwenye maeneo ya makazi na yanayotumika kwa shughuli za kijamii hususani biashara kunaleta sura mbaya kwa chama kwakuwa kunahatarisha afya za watekelezaji wa Ilani.

Na Joachim Nyambo,Mbeya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527