TUME YA TAIFA YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA (COSTECH" KUANZISHA KIOTA 'HUB' MKOANI NJOMBE KUWEZESHA WABUNIFU


Mbunifu Railes Ngailo akimweleza NaibuKatibu Mkuu Wizaza ya Maji Mhandisi Emanuel kalobelo changamoto ya Nguzo na nyaya anazozitumia .
Naibu Katibu Mkuu Wizaza ya Maji Mhandisi Emanuel kalobelo akishangazwa na Mfumo wa uzalishaji wa Umeme wa Mbunifu John Fute (Mzee Pwagu).
NaibuKatibu Mkuu Wizaza ya Maji Mhandisi Emanuel kalobelo akitoa agizo kwa wahandisi wa maji nchini kuhakikisha wanatambua vyanzo vya maji vinavyoweza kutumia Pampu za Mbunifu John Fute (Mzee Pwagu).
Mhandisi Pakaya Mtamakaya kutoka TANESCO Makao Makuu akimweleza NaibuKatibu Mkuu Wizaza ya Maji kuwa wameona fursa kwa wabunifu hao.
Mfumo wa Usambazaji wa umeme anaoutumia Mbunifu Railes Ngailo.

Tume ya Taifa ya sayansi na Teknolojia (COSTECH) imeahidi kuanzisha kiota (HUB) mkoani Njombe ili kuwawezesha wabunifu wa mkoa huo kupatiwa mafunzo ili kuendeleza bunifu zao,akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume Ndugu Deusidedith Leonard amesema tayari wameanzisha kumbi kama hizo katika Mkoa wa Iringa ambazo ni KIOTA HUB na R-HUB ambazo kwa kuanzia wataalam wake wanaweza kutumiwa kuwafundisha wabunifu hao.

Hayo ameyasema Mkoani Njombe alipofika kwa ajili ya kuwaona na kuwatambua wabunifu wa kuzalisha umeme wa maji mkoani humo ambao ni Ndugu JOHN FUTE (Mzee Pwagu) na RAILES NGAILO ikiwa ni utekelezaji wa agizo la mheshimiwa Raisi alilolitoa katika hafla iliyofanyika Ikulu tarehe 13/06/2019.

Alisema kuwa, kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa na wilaya ya Njombe ambao watatoa ukumbi na mtu wakupatiwa mafunzo ya namna ya kuendesha “HUB” wataweza kuwasaidia wabunifu hao kujengewa uwezo ili waweze kuwa wajasiriamali na wafaidike na Bunifu zao.

Aliongeza kuwa ahadi waliyoitoa kwa Mheshimiwa Rais Dkt JOHN MAGUFULI ya kuwakabidhi kiasi cha shillingi Milioni kumi kila mmoja, ilitimizwa tarehe 14 Juni 2019 katika ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania TBC, MIKOCHENI jijini Dares Salaam.

Pia, mwakilishi wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Bi. MARGARETH KOMBA alitoa wito kwa Viongozi wa wilaya zote kuhakikisha wanatoa ushirikiano katika kuwatambua wabunifu walioko katika maeneo mbalimbali ili waweze kufikiwa kwa haraka.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi EMMANUEL KALOBELO ameona fursa kwenye Pampu za maji anazozitengenezwa na Mzee FUTE kwamba zinaweza kusaidia kuzalisha maji kwenye maeneo mengi vijijini na kuokoa garama kubwa ambayo Serikali inatumia katika miradi ya maji vijijini, amesema kitendo hicho kitatoa hamasa kwa wabunifu wote nchini kuona serikali yao inawajali na kutambua mchango wao katika kuletea taifa maendeleo.

Vilevile, akatoa agizo kwa Waandisi wa Mkoa wa Njombe kuhakikisha wanatambua maeneo yote yanayoweza kutumika katika kuzalisha maji kwa kutumia Pampu za Mzee FUTE na kumpelekea taarifa mapema.

Wakati huo huo Mhadisi KALOBELO aliagiza kuondolewa kwenye nafasi Mhandisi wa maji Mkoa wa Njombe(…) kwa kushindwa kutambua na kutimiza majukumu yake na kutaka apangiwe nafasi nyingine inayoendana na uwezo wake.

Kwa upande wa TANESCO Mhandisi PAKAYA MTAMAKAYA amesema wameona fursa na wanaendelea kufanya upembuzi yakinifu na kuhakikisha wanakuja na ripoti nzuri itakayosaidia kuboresha umeme wa wabunifu hao.

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Katibu tawala wa Mkoa wa Njombe Bw. CHARLES KICHERE amemshukuru mheshimiwa Rais kwa kutambua umuhimu wa wabunifu hao ambao wameupa heshima kubwa mkoa wa Njombe na kuahidi kufuatilia kwa ukaribu maendeleo yao.

Nao wabunifu hao wameishukuru COSTECH, TANESCO, Wizara ya Maji na REA kwa kutekeleza agizo la Rais Dkt JOHN MAGUFULI la kuwatambua na kuwawezesha katika kuongeza ufanisi kwenye kazi zao ambao utapelekea kunufaisha wakazi wa vijiji vyao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527