Zaidi ya Shilingi Bilioni 253 kuibeba Sekta ya Kilimo

Na Mathias Canal
Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga  tarehe 17 Mei 2019 ameliomba Bunge kulidhia na kupitisha kiasi cha Shilingi Bilioni 253 kwa ajili ya kugharamia matumizi ya kawaida na miradi mbalimbali ya maendeleo ya Sekta ya Kilimo kwa mwaka wa Fedha wa 2018/2019.

Akisoma Bajeti kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Fedha za Wizara ya Kilimo kwa Mwaka 2019/2020, Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga amesema, Serikali imepanga kubadilisha kilimo kutoka kuwa cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Aidha, Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo umesisitizia mapinduzi ya viwanda na umeitambua Sekta ya Kilimo kuwa mhimili imara kwa ajili ya upatikanaji wa malighafi za viwanda. Miongozo hiyo ya Kitaifa, pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na Sera ya Kilimo ya mwaka 2013, inatekelezwa na Wizara kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ambayo inalenga kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo na kwa kutambua umuhimu wa kuongeza mitaji, teknolojia na ubunifu, Sekta Binafsi inashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa ASDP II.

Mhe. Hasunga ameongeza kuwa Fedha nyingi katika kiasi hicho cha Bilioni 253 zitaelekezwa kwenye utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) iliyozinduliwa rasmi tarehe 4 Juni, 2018 na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inalenga kubadilisha maisha ya mkulima kwa kufanya mageuzi makubwa kwenye kilimo kwa kuzingatia mazao ya kipaumbele kulingana na ikolojia za kilimo.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa chakula katika mwaka 2018/2019 Waziri Hasunga amesema upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2018/2019 ulifikia tani milioni 16.89 zikiwemo tani milioni 9.53 za mazao ya nafaka na tani milioni 7.35 za mazao yasiyo nafaka. Kiwango hicho cha uzalishaji kimeiwezesha nchi kujitosheleza kwa mahitaji yake ya chakula ya tani milioni 13.56 na hivyo kuwa na ziada ya tani milioni 3.32 za chakula kwa kiwango cha utoshelevu cha asilimia 124.

“Niwahakikishie watanzania kwamba, tunacho chakula cha kutosha nchini. Hata hivyo, tuendelee kuweka akiba katika kaya zetu hadi tutakapovuna tena kwani inaonekana kwamba huenda tusiwe na mavuno mazuri sana msimu huu kutokana na uhaba wa mvua kwenye maeneo ya Kanda ya Ziwa, Kati na Kaskazini mwa nchi yetu”. Amekaririwa Waziri Hasunga.

Kuhusu kilimo cha umwagiliaji, Mhe. Hasunga amesema katika mwaka 2018/2019, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imekamilisha mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 ili kubaini maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa kuzingatia Mipango Shirikishi ya Maendeleo ya Rasilimali za Maji. Katika mpango huo, hekta 560,880 zimepangwa kuendelezwa kwa lengo la kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 475,052 mwaka 2018/2019 hadi hekta 1,000,000 ifikapo mwaka 2035.

Waziri Hasunga ameuzungumzia Ushirika na kusema Wizara kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeendelea kuimarisha Sekta ya Ushirika kwa kusimamia na kuhamasisha maendeleo yake. Vyama vya Ushirika vimeongezeka kutoka vyama 10,990 Desemba 2017 hadi vyama 11,331 kufikia Desemba 2018. Vilevile, idadi ya wanachama wa vyama vya ushirika imeongezeka kutoka 2,619,311 mwaka 2017 hadi 3,998,193 Februari, 2019 sawa na ongezeko la asilimia 53.

Hadi Desemba 2018, mikopo yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.3 imetolewa kwa wanachama ikilinganishwa na Shilingi bilioni 902 iliyotolewa kufikia Desemba 2017.Aidha, Akiba na Amana za wanachama katika SACCOS zimefikia Shilingi bilioni 575 na hisa Shilingi bilioni 79.

Bunge litaendelea kujadili hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya Mwaka 2018/2019 kwa siku mbili ambapo Jumatatu tarehe 20 Mei, 2019 inakuwa siku ya kuhitimisha majadiliano hayo na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Fedha za Wizara ya Kilimo kwa Mwaka 2019/2020


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post