WATU 80 WAMEMATWA NIGERIA KWA TUHUMA ZA KULA WAKATI WA RAMADHAN

Polisi katika Jimbo la Kano, kaskazini mwa Nigeria wamewakamata kwa muda watu 80 waliotuhumiwa kwa kula hadharani badala ya kufunga kuanzia alfajiri hadi jua linapotua kulingana na maagizo ya dini ya Kiislamu katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.


Polisi wa Sharia, wanaofahamika kama Hisbah, wanasema kuwa watu hao walikamatwa kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali ya mji wa Kano katika kipindi cha siku kadhaa.

Jimbo la Kano ni moja kati ya majimbo kadhaa ya kaskazini mwa Nigeria ambako Sharia ya Kiislamu ilianzishwa upya tangu mwaka 2000.

Sharia ya Kiislamu inatekelezwa sambamba na sheria ya kawaida kwenye majimbo hayo.

Msemaji wa Hisbah katika jimbo la Kano, Adamu Yahaya ameiambia BBC kuwa wote waliokamatwa walikuwa ni Waislamu na maofisa hawawalengi wasio Waislamu kwa sababu hawafungwi na sheria ya Kiislamu.

Amesema kuwa baadhi ya wale waliokamatwa waliiambia ofisi ya Sharia kuwa walikuwa wanakula kwa sababu hawakuona binafsi mwezi, huku wengine wakisema walikuwa ni wagonjwa, lakini maofisa walisema kuwa madai yao hayakuwa na msingi wowote.

Watu hao 80 walionywa na kuachiliwa huru kwa sababu walikuwa wamefanya kosa hilo kwa ''mara ya kwanza'' alisema Yahaya.

Walionywa kuwa iwapo watakamatwa tena, watapelekwa mahakamani.

Hisbah wamesema kuwa wataendelea kufanya doria katika kipindi chote cha Ramadhani kwa lengo la kuwakamata Waislamu wote ambao hawafungi katika mwezi huu.

Mfungo wa Ramadhani ni lazima kwa kila mtu mzima Mwislamu, lakini baadhi ya watu kama vile wagonjwa  hawatakiwi kufunga.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527