WAANDISHI WA HABARI IRINGA WAMKALIA KOONI MKUU WA MKOA...WAMTAKA AOMBE RADHI

Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa wamempa siku saba mkuu wa Mkoa huo, Ally Hapi kuwaomba radhi baada ya kuwataka nao kuwa na vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo.

Hapi alitoa kauli hiyo juzi Jumatatu Mei 27, 2019 wakati akizungumza na watendaji wa Serikali kuhusu ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara.

Aliwataja waandishi wa habari kama wafanyabiashara na vibarua wasio rasmi, huku akianisha makundi 53 yanayostahili kupata vitambulisho hivyo.

“Wafanyabiashara ni wengi kuna wapiga debe, wauza nyanya, mchicha, wachoma mahindi na hata waandishi wa habari na wapiga picha wote wanatakiwa kuwa na vitambulisho ili kuchangia kodi kutokana na kazi wanazofanya,” amesema Hapi.

Akizungumza jana  Jumanne Mei 28, 2019 mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Iringa, Frank Leornald amesema kauli ya Hapi inadhalilisha taaluma ya habari.

Leornald amesema waandishi wa habari mkoani humo wamefanya majadiliano na kuazimia mambo sita watakayoyawasilisha katika ofisi ya mkuu huyo wa Mkoa, na kutaka majibu ya haraka.

“Tumesikitishwa kuwekwa katika kundi moja linalolinganisha taaluma ya habari na wafanyabiashara. Katika maazimio hayo sita tumemuomba Hapi kutoa tafsiri rasmi anayoijua yeye kuhusu waandishi rasmi na wasio rasmi.”

“Tunaamini taaluma ya habari ni kama taaluma nyingine za sheria, udaktari na ualimu hivyo kuingiza wanahabari katika kundi la wafanyabiashara wanaotakiwa kuwa na hivyo vitambulisho ni kuidhalilisha taaluma yetu,” amesema Leornald.

Amebainisha kuwa Hapi anapaswa kuomba radhi kutokana na kauli yake hiyo.

“Mengine tutayatolea uamuzi baada ya Hapi kujibu barua yetu tuliyomuandikia,” amesema Leornald.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527