TANZANIA KUWA MWENYEJI WA ZOEZI LA KUPIMA UTAYARI WA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO MIPAKANI KWA DHANA YA AFYA MOJA


Kufuatia nchi za Kanda ya Afrika Mashariki kuwa katika hatari ya kuathirika na magonjwa ya mlipuko kama Homa ya Bonde la Ufa, Mafua Makali ya Ndege na Ebola, na kwa kuwa magonjwa hayo husambaa kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine, Tanzania inatarajia kuandaa zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, litakalofanyika mpakani mwa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga,  kuanzia tarehe 11 hadi 14 Juni mwaka huu.

Zoezi hilo, litazingatia Dhana ya Afya moja ambayo hujumuisha sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo na  mazingira katika kujiandaa, kufuatilia  na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu. Jumla ya washiriki 150 ambao watatoka Sekretarieti ya Afrika Mashariki, Kenya na Tanzania washiriki 130 kutoka ngazi ya taifa, mkoa na wilaya katika mpaka wa Namanga; pamoja na nchi nyingine wanachama ambapo watakuwa watazamaji ikiwa ni Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani Kusini wanatarajiwa kushiriki zoezi hilo.

Akiongea, mjini Dodoma leo, katika kikao cha maandalizi ya zoezi hilo kwa ngazi ya Taifa, Mkurugenzi wa Kitengo cha Dharura na Majanga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Dkt. Eliasi Kwesi,  amefafanua kuwa zoezi  hilo linalenga kufanyia majaribio ya utekelezaji wa Mipango ya Dharura ya Taifa na Kanda, Miongozo ya Utendaji na kuwapa washiriki fursa ya kujifunza namna sekta zingine zinavyotekeleza majukumu katika kuzuia na kupunguza madhara pamoja na kujiandaa kukabiliana na maafa ya magonjwa ya mlipuko.

“Zoezi hili tunalenga kutathmini utaratibu wa kutuma kikosi cha taifa cha dharura cha kukabili lakini pia  kuhakiki matumizi ya maabara zinazohamishika, kutathmini uwezo wa uchunguzi na usimamizi wa magonjwa ya mlipuko kwa vituo vilivyopo mpakani kwa magonjwa ya mifugo na binadamu; kupima hatua za kujiandaa kukabiliana katika viwanja vya kimataifa vya Jomo Kenyatta na Kilimanjaro.” Alisisitiza Dkt. Kwesi.

Kwesi alibainisha kuwa zoezi litaandaliwa kwa kuhusisha mlipuko wa virusi vinavyoshabihiana na Homa ya Bonde la Ufa katika eneo la mpakani, ambapo washiriki watahitajika kuonesha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo kwa kuzingatia mfumo wa Afya Moja.

Zoezi hilo linafanyika nchini Tanzania kufuatia Kikao cha 11 cha Kawaida cha Mawaziri wa Sekta ya Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika mwezi Machi, 2015, ambapo kilielekeza Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuandaa Zoezi la Nadharia la kukabiliana na magonjwa ya mlipuko katika mpaka wa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga. Zoezi hilo ambalo litafanyika hapa nchini  linaratibiwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na nchi wanachama kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani la GIZ na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post