MWENYEKITI WA BUNGE AISHAURI SERIKALI KUWA NA MTAALA MMOJA WA ELIMU KWA PANDE ZOTE MBILI ZA MUUNGANO

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma

Mwenyekiti wa Bunge La Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Nagma Giga ameishauri serikali ya  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Tanzania bara kukaa pamoja kuona namna ya kuwa na Mtaala mmoja wa Elimu ili kuinua na kuboresha kiwango cha ufaulu kwa pande zote mbili.

Mhe.Giga amesema hayo leo Mei 22,2019 Bungeni jijini Dodoma wakati akielekeza swali la nyongeza kwa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambapo amesema pamekuwepo na mkanganyiko mkubwa katika suala la Elimu kwa Zanzibar na Tanzania Bara kutokana na Mitaala ya Elimu kutofautiana hali ambayo husababisha Zanzibar kuwa nyuma.

Akijibu Swali hilo Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia ,Mhe.Wiliam Ole Nasha amesema serikali itaangalia namna ya kufanya ili kuweza kutoa mitaala ya elimu inayofanana ili kuondoa mkanganyiko kwa pande zote mbili za Muungano kati ya Tanzania bara na Zanzibar.

Aidha.Mhe.Wiliam Ole Nasha amesema serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali  ili kuongeza ufaulu katika ngazi mbalimbali za elimu ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundo mbinu  ambapo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/209 zaidi ya Tsh.  Bilioni 93.8  zimetumika kuboreha miundombinu  ya shule 588.

Pia amesema  serikali imeendelea kuimarisha  Idara ya Uthibiti  Ubora wa shule  ambapo imenunua na kusambaza magari 45  ya uthibiti Ubora  wa shule na pikipiki 2,897 kwa ajili ya Maafisa Elimu Kata kwa mwaka 2019/2020  huku ikitarajia kujenga ofisi 100  za wathibiti Ubora   wa Shule  na kuongeza idadi ya watumishi.

Ikumbukwe kuwa ufaulu wa wanafunzi katika kidato cha nne  umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka  ambapo mwaka 2018   asilimia 78.36% ya watahiniwa walifaulu  ikilinganishwa  na 77.09 %  ya mwaka 2017 ,70.35 %ya mwaka 2016 na 67.91 % ya mwaka 2015.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post