SPIKA NDUGAI ATANGAZA KUSITISHA UWAKILISHI WA MBUNGE MASELE KWENYE BUNGE LA AFRIKA (PAP),MWENYEWE AENDELEA NA KIKAO KAMA KAWAIDA (Picha).


Makamu wa rais wa Kwanza wa rais wa Bunge la Afrika,Mhe. Stephen Masele akiendelea na shughuli za bunge la Afrika leo,juu ni Rais wa Bunge la Afrika,Mhe. Roger Nkodo Dang akiendesha kikao cha bunge.
Bunge la Afrika likiendelea leo.
Stephen Masele (kushoto) na Spika Job Ndugai (kulia).

Wakati Sintofahamu ikitokea katika bunge la Afrika (Pan- African Parliament - PAP),Spika wa bunge la Tanzania Job Ndugai ametangaza kusitisha uwakilishi wa Mbunge Stephen Masele kwenye Bunge la Afrika (PAP) ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge hilo kwa tuhuma za utovu wa nidhamu mpaka atakapohojiwa na Kamati ya Maadili ya Bunge.

Ndugai ametangaza uamuzi huo leo Alhamisi, Mei 16, 2019 wakati akizungumza bungeni jijini Dodoma.

“Tunao wabunge wanaotuwakilisha kwenye mabunge mbalimbali ya Afrika ikiwemo SADC, Pan African Parliament (PAP), African Caribbean Pacific, Bunge la Afrika Mashariki na Bunge la Maziwa Makuu, wamekuwa wakifanya vizuri katika kutuwakilisha.

“Lakini katika Bunge la Afrika (PAP) kumetokea matatizo makubwa hasa kwa Mheshimiwa Stephen Masele ambayo nisingependa kuyafafanua kwa sababu muda hautoshi, tumelazimika kumtafuta na kumrudisha nyumbani kuanzia Jumatatu lakini ameonyesha kugoma.

“Baada ya kumwandikia barua arudi nyumbani aje kwenye kamati yetu ya maadili, jana wakati akihutubia bunge hilo alisema japo ameitwa na spika, lakini waziri mkuu amemwambia abaki na aendelee na mambo yake, kitu ambacho ni uongo na anatudhalilisha kama nchi.

“Masele ni kiongozi ambaye amekuwa akifanya mambo ya hovyohovyo, ndiyo maana tumemuita atufafanulie huenda yuko sahihi, lakini anafanya mambo ambayo ni hatari kubwa, amejisahau sana, amekuwa akichonganisha mihimili ya Serikali tena ya juu kabisa, hajui hata anatafuta nini.

"Kwa kuwa hataki kuja, nimemwandikia barua Rais wa PAP (Roger Nkodo Dang) ya kusitisha uwakilishi wa Mheshimiwa Masele kwenye bunge la PAP, hadi Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge itakapomalizana naye hapa. Pia, kamati ya maadili ya chama chake (CCM). Kwa hiyo kuanzia sasa siyo mbunge tena wa PAP mpaka tutakapomalizana naye hapa nyumbani,” amesema Ndugai.

Uamuzi wa Spika Ndugai imekuja wakati Kamati Maalumu ya kuchunguza tuhuma dhidi ya rais wa bunge la Afrika, Mhe. Roger Nkodo Dang iliyoundwa na wabunge wa bunge la Afrika (PAP)   za unyanyasi wa kingono kwa watumishi wa kike walioko Makao Makuu ya PAP walivyonyanyaswa kingono bila ridhaa yao, matumizi mabaya ya madaraka, upendeleo ndani ya bunge hilo na unyanyasaji kwa watumishi wa ofisi hiyo hali iliyosababisha kuwepo kwa mgomo wa watumishi wa Bunge.

Habari kutoka katika bunge la Afrika zinaeleza kuwa Masele ambaye ni makamu wa kwanza wa Rais wa PAP amekuwa hapatani na Rais wa PAP, mhe.Nkodo kwa madai kuwa Nkodo amekuwa akikiuka kanuni za bunge la Afrika hivyo,kitendo cha kutaka aondoke katika bunge la Afrika ni hujuma anazofanyiwa.

Miongoni mwa vitendo vya ukiukwaji huo wa kanuni ni mhe.Nkodo kuleta wabunge saba kutoka nchi ya Cote di'voire badala ya watano kama inavyotakiwa kila nchi.

Akiongoza kikao cha bunge,siku moja baada ya wabunge hao kuapishwa, Masele aliwatimua bungeni wabunge wawili walioongezeka na kubakiza watano kwa mujibu wa kanuni za bunge hilo, kitendo ambacho kinaelezwa kumkera rais wa PAP,Roger Nkodo Dang ndipo mvutano kati yake na Masele anayeungwa mkono na wabunge wengi kwenye bunge hilo ulipoanza bungeni huku hofu ya Nkodo kupoteza kiti cha urais ikitawala na kulazimika kutumia kila mbinu kujinasua.

Kutokana na tuhuma mbalimbali dhidi ya Rais wa PAP, Mhe.Nkodo  wafanyakazi wa bunge la Afrika wiki iliyopita waligoma kufanyakazi wakati bunge linaendelea,hali iliyomlazimu Rais kuahirisha bunge ili uongozi wa kamati ya bunge ukutane na wafanyakazi kutatua mgogoro huo uliojitokeza.

Baada ya kukutana na wafanyakazi,ziliibuka tuhuma mbalimbali dhidi ya rais Nkodo, hivyo wabunge wakakubaliana kuunda kamati maalumu kuchunguza tuhuma dhidi ya rais wa PAP iliyotakiwa kutoa ripoti jana Mei 15,2019 lakini ikaomba itoe ripoti leo Alhamis kutokana na kutokamilisha uchunguzi kwani kamati ilikuwa haijamhoji mtuhumiwa Nkodo.

Hata hivyo jana asubuhi,wakati kikao cha bunge kikianza,rais wa PAP,Mhe. Nkodo aliliambia bunge hilo kuwa amepokea barua kutoka kwa Spika wa bunge la Tanzania Mhe. Job Ndugai kuwa,Masele anatakiwa arudi nyumbani kitendo ambacho kilipingwa na Masele pamoja na wabunge wa bunge la Afrika wakisema Masele hawezi kutoka bungeni wakimtaka rais afute hiyo hoja,ndipo akaiondoa na Masele akaendelea kushiriki vikao vya bunge hilo.

"Mheshimiwa Rais najua ulichokusudia kufanya, lakini huwezi kufanya hivyo unavyotaka. Ni kinyume cha sheria. Bunge la Afrika lina itifaki na miiko yake. Kama unadhani nitakaa hapa na kuongea yale unayotaka kusikia, mimi si mwanaume wa aina hiyo.

Nitakueleza uhalisia wa kile ninachokiona",alisema Masele huku akipigiwa makofi na wabunge.

Inadaiwa kuwa anayetakiwa kuongoza kikao cha bunge la Afrika wakati kamati maalumu iliyoundwa kuchunguza tuhuma dhidi ya rais wa PAP Mhe.Nkodo, ikiwasilisha ripoti hiyo ni Mhe. Masele, huku ikielezwa kuwa rais wa PAP hataki Masele awepo bungeni.

Ripoti ya kamati hiyo itatolewa leo mchana kwenye kikao cha bunge la Afrika kinachoendelea nchini Afrika Kusini ambapo Mhe.Masele anaendelea kushiriki shughuli za bunge kama kawaida.

Mkutano wa bunge la Afrika utafungwa kesho Ijumaa Mei 17,2019.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post