SERIKALI KUENDELEA KUTOA ELIMU YA MATUMIZI YA MBOLEA YA ASILI

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Serikali kwa kushirikiana na taasisi za sekta binafsi imeendelea kutoa elimu ya kilimo bora inayojumuisha matumizi sahihi ya mbolea za asili, viuatilifu vya asili, mbegu bora na hifadhi ya mazingira ili kuzalisha mazao kwa tija na kuwa na kilimo endelevu.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 8 Mei 2019 wakati akijibu swali la Mbunge wa Chambani Mhe Yussuf Salim Hussein aliyetaka kufahamu Serikali imeweka mikakati gani ya kutoa elimu ya mbolea ya asili kwa wakulima na hatua Serikali inayoichukua ili kuona kuwa Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kuzalisha mazao yasiyotumia mbolea za viwandani.

Alisema kuwa katika kutekeleza mpango wa muda mrefu wa matumizi sahihi ya virutubisho vya udongo, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) inafanya utafiti wa afya ya udongo katika Kanda zote saba za kiikolojia za kilimo nchini.

Utafiti huo unalenga kubaini aina za virutubisho na tabia za udongo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuweza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kiasi, aina na matumizi sahihi ya mbolea za viwandani na asili. Utafiti huo umeanza kwa kuchukua sampuli za udongo katika Kanda za Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini na sehemu ya Kanda ya Mashariki (Mkoa wa Morogoro) na utaendelea katika maeneo mengine nchini na kukamilika Juni 2020.

Alisema, kwa kutambua ongezeko la mahitaji ya mazao na bidhaa za kilimo zinazozalishwa kwa kutumia mbolea za asili na viuatilifu vya asili, Serikali imeboresha mtaala wa mafunzo katika vyuo vya kilimo ambapo mada za kilimo hai na hifadhi ya mazingira zimejumuishwa ili kuwawezesha maafisa ugani na wakulima kupata elimu hiyo.

Mhe Mgumba aliongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Tanzania Organic Agriculture Movemet (TOAM), Sustainable Agriculture Tanzania (SAT), Ecology Agriculture chini ya SWISSAID, Zanzibar Organic Producers (ZANOP), Tanzania Alliance for Biodiversity (TABIO) na TANCERT inatoa elimu ya kilimo hai kwa wakulima na kutoa vyeti vya ubora wa mazao kwa ajili ya masoko maalum. Baadhi ya mazao ambayo yanazalishwa katika mfumo wa kilimo hai hapa nchini ni pamoja na kakao, kahawa, pamba na viungo.

Kadhalika, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe Easter Michael Mmasi aliyetaka kufahamu kuhusu ushiriki wa wanawake kwenye sekta ya kilimo, Mhe Mgumba alisema kuwa Sekta ya Kilimo inajumuisha sekta ndogo za kilimo mazao, mifugo, uvuvi na misitu.

Bajeti za Wizara za Sekta ya Kilimo zinajumuisha bajeti za Wizara za sekta husika, Bodi za mazao na Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara za Kisekta. Utekelezaji wa bajeti hizo huwawezesha  wanaume na wanawake katika shughuli za kilimo. Wanawake wanachangia asilimia 90.4 ya nguvukazi ya wanawake inayotumika katika shughuli za kilimo na kuchangia wastani wa asilimia 70 ya mahitaji ya chakula nchini. 

Mhe Mgumba alisema kuwa katika kutatua changamoto hizo Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 kupitia mifuko ya uwezeshaji ikiwemo Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake (Women Development Fund - WDF) ambao huchangiwa asilimia 4 ya mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kila mwaka. Katika mwaka 2017/2018, jumla ya Shilingi 15,633,312,764.91 zimetolewa kwa vikundi 2,919 vya wanawake na vijana vyenye jumla ya wanawake wajasiriamali 29,190 katika Halmashauri mbalimbali nchini.

Aidha, alisema kutokana na umuhimu wa wanawake katika kilimo Serikali imeielekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo (Tanzania Agricultural Development Bank – TADB) katika mikopo inayotoa asilimia 20 ya mikopo itolewe kwa vikundi vya wanawake. Hadi Januari 2019, asilimia 33 ya mikopo imetolewa katika vikundi vya wanawake kupitia Benki ya TADB. Vilevile, benki za NMB na Azania zimeanzisha dirisha maalumu la kutoa mikopo kwa vikundi vinavyo jishughulisha na kilimo na miradi mbalimbali. Pia Serikali imehamasisha wanawake kujiunga kwenye vikundi vya ushirika wa akiba na mikopo kama SACCOS, VICOBA ili kupata huduma za kifedha na mikopo kwa urahisi ili kuongeza mitaji yao katika kilimo.

Mhe Mgumba aliongeza kuwa, Serikali imeuelekeza Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (Agricultural Input Trust Fund - AGITF) kutoa kipaumbele kwa vikundi vya wanawake vinavyoomba mikopo ya kuendeleza kilimo. Vile vile, Serikali imeendelea kutoa hati miliki za ardhi za kimila na hati miliki za ardhi kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kumiliki ardhi na kuzitumia kama dhamana kukopa katika taasisi mbalimbali za kifedha ili waweze kupata mitaji ya kununua pembejeo na zana bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji, tija na kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya usindikaji wa mazao ya kilimo.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527