RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA AMLILIA DR. REGINALD MENGI


Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa ametuma salamu zake  za Rambi Rambi Kufuatia Kifo Cha Dkt Reginald Mengi  akisema Mengi alikuwa miongoni mwa Watanzania wachache waliokuwa wazalendo ambao Taifa halitawasahau.

“Nimemfahamu Mengi miaka mingi iliyopita na kwangu ananirudisha katika historia kama mzalendo aliyesimamia nafasi yake kwa jamii,” alisema Mkapa kupitia ujumbe wake wa rambirambi .

Alimtaja Mengi kuwa ni kati ya wazalendo wachache walioanzisha viwanda, aliyejitolea kwa ajili ya maisha ya wengine na kupambana kuondokana na umaskini ambaye Taifa litaendelea kujivunia.

“Wakati wa urais wangu, Dk Mengi kupitia shughuli mbalimbali alinifanya niwe Rais mzuri. Alikuwa mkweli katika maoni yake hata kama yalikuwa tofauti na misimamo yangu na hilo lilinifanya kufaidika na busara zake,” alisema Rais huyo mstaafu.

Alisema utumishi wa Mengi katika sekta binafsi umeendelea kuilea hadi leo na anatambulika kama mtu aliyemshawishi kila anayetamani kuona nchi ikiendelea.

Alisema namna pekee ya kumuenzi ni kufuata njia na mifano aliyoionyesha, kwamba kupambana na umaskini siyo jukumu la Serikali peke yake bali ni la kila mtu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post