POLISI NA ASKARI MAGEREZA WAPIGANA MAKONDE HADHARANI, MABOMU NA RISASI ZARINDIMA STENDI YA MABASI


Polisi na Askari wa Jeshi la Magereza wilayani Masasi Mkoani Mtwara, wamepigana makonde hadharani katika eneo la stendi kuu ya mabasi barabara kuu iendayo Tunduru.Akizungumzia tukio hilo,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Blasius Chatanda, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 6 mchana baada ya askari polisi kumkamata askari Magereza ambaye inadaiwa alikuwa anaendesha pikipiki bila ya kuvaa kofia ngumu.

Hata hivyo, Kamanda Chatanda hakutaja majina ya askari huyo na polisi.

Chatanda alisema baada ya kutokea kwa ugomvi huo, Polisi walifyatua risasi hewani na kurusha mabomu ya machozi hali ambayo ilisababisha taharuki kubwa kwa wananchi wilayani humo.

Alisema muda kidogo walitokea askari Magereza watano ambao walifika eneo la tukio kwa ajili ya kumuokoa mwenzao, ndipo polisi na askari wa Magereza walipoanza kupigana.

Kamanda Chatanda alisema polisi huyo alikuwa doria katika operesheni ya kawaida ya ukamataji wa vyombo vya moto hasa pikipiki maarufu kama bodaboda, ambao wamekuwa wakiendesha bila ya kufuata sheria za usalama barabarani.

Alisema baada ya Polisi huyo kumshika askari magereza ambaye alikuwa kiendesha pikipiki bila ya kuvaa kofia ngumu na kumtaka kwenda kituo cha polisi au kuiacha pikipiki yake, alipinga ndipo mzozo ulipoanza.

“Baada ya muda kidogo kundi la askari magereza walifika kumuokoa mwenzao mara baada ya kumuona ameshikwa na Polisi, pia kundi la askari polisi walifika nao kumuokoa mwenzao, ndipo makundi hayo mawili ya jeshi walipoanza kuchapana makonde na kufyatua risasi hewani,” alisema Kamanda Chatanda.

Kamanda Chatanda alisema kufuatia tukio hilo, Jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa kujua chanzo zaidi ya vurugu hizo ikiwamo kufanya vikao vya dharura kati ya Jeshi la Polisi na Magereza, na kwamba uchunguzi utakapokamilika sheria itachukua mkondo wake.


Chanzo: Nipashe.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post