WATAHINIWA 91,442 KUFANYA MTIHANI WA KIDATO CHA SITA KUANZIA KESHO

 Watahiniwa 91,442 wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kumaliza kidato cha sita kuanzia kesho Jumatatu Mei 6 hadi 23, 2019.

Mbali na hao, watahiniwa 12,540 wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kumaliza kozi ya ualimu katika ngazi ya cheti na stashahada.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Mei 5, 2019 Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde, amesema kumekuwa na ongezeko la watahiniwa wa shule wanaomaliza mtihani wa kidato cha sita kwa asilimia 4 ikilinganishwa na mwaka jana huku idadi ya watahiniwa wa ngazi ya ualimu wakiongezeka kwa asilimia 41.

“Mwaka jana watahiniwa wa shule waliosajiliwa walikuwa 77,222 na watahiniwa katika ngazi ya ualimu waliosajiliwa mwaka huo walikuwa 7,422,” amesema Dk Msonde.

Akitoa ufafanuzi wa watahiniwa wa mtihani wa kidato cha sita waliosajiliwa mwaka huu, amesema kati 80,305 ni watahiniwa wa shule na 11,117 ni wa kujitegemea

“Katika watahiniwa wa shule kati yao 46,224 sawa na asilimia 57.56 ni wavulana na 34,081 sawa na asilimia 42.44 ni wasichana huku watahiniwa walio na uhitaji maalumu wapo 102 kati yao, 67 ni wenye uoni hafifu; 16 ni wasioona; 18 wenye ulemavu wa kusikia; na 1 ni mwenye ulemavu wa afya ya akili,” amesema Dk Msonde.

Katika watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa 7,190 kati yao sawa na asilimia 64.68 ni wavulana, ni 3,927 wasichana sawa na asilimia 35.32.

Pia, katika watahiniwa wanaotarajiwa kufanya kozi ya kumaliza ualimu kati yao 7,594 ni ngazi ya stashahada na 4,946 ngazi ya cheti.

“Katika watahiniwa wa ngazi ya stashahada waliosajiliwa kati yao 5,615 sawa ana asilimia 74 ni wavulana; na 1,979 sawa na asilimia 26 ni wasichana.

“Na watahiniwa waliosajiliwa katika ngazi ya cheti waliosajiliwa 2,795 sawa na asilimia 57 ni wavulana na 2,151 sawa na asilimia 43 ni wasichana,” amesema Dk Msonde.
Na Aurea Simtowe - Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527