UGOMVI WA WANANDOA WAUNGUZA NYUMBA 300 KIBERA

Haijulikani chanzo cha ugomvi wenyewe, lakini matokeo ya ugomvi huo yamezua hasara kubwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya gazeti la Star la nchini Kenya, ugomvi wa wanandoa hao uliotokea Jumanne usiku ulianzia kwa maneno na kisha kuvaana mwilini, katika purukushani hizo, jiko lao la gesi likadondoka na kulipuka.

Moto ukatanda ndani ya nyumba yao, na baada ya muda mfupi ukazikumba nyumba nyingine pia.

Eneo ulipozuka moto huo ni kitongoji maarufu cha Kibera jijini Nairobi ambacho wakaazi wake ni masikini sana.

Makaazi katika eneo hilo hayajapangiliwa na nyumba zimekaribiana sana, hivyo linapotokea janga la moto, ni kawaida kwa zaidi ya nyumba moja kuathirika.

Hata hivyo, si jambo la kawaida kwa moto kuunguza nyumba mpaka 300, na kuacha maelfu ya wakaazi bila makao.Kitongoji cha Kibera ni moja ya maeneo wanayokaa watu masikini Nairobi na makazi yake hayajapangiliwa.

Mamlaka zimeamua kuficha utambulisho wa wanandoa hao kwa makusudi ili kuwalinda dhidi ya ghadabu ya wakaazi wengine ambao wamethirika pakubwa.

Eneo liliotokea moto huo linaitwa laini saba na tayari mwakilishi wake kwenye bunge la Kaunti ya Nairobi Cecilia Ayot amesema mvua zimefanya hali izidi kuwa mbaya.

"Watu wameachwa bila makazi. Bahati mbaya zaidi ni kuwa kwa mvua zinazoendelea, hata ile sehemu ambayo walikuwa wanajihifadhi haipo tena," amesema Ayot.

Mwakilishi huyo pia amekemea vikali ukatili wa majumbani na ugomvi: "Kuna namna nyingi za kutatua matatizo, na ugomvi si jia muafaka ya kufanya hivyo. Watu (wanaogombana) inawapasa waombe ushauri na usuluhishi badala ya kupigana, tumeona madhara ya ugomvi na jinsi ulivyoathiri maisha ya maelfu ya watu kwa kuteketeza nyumba 300.

Kikosi cha zimamoto cha jiji la Nairobi kimejitetea kuwa ujenzi wa kiholela katika eneo hilo uliwazuia kulifikia eneo hilo na kuuzima moto kwa haraka.
Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post