MDUDE WA CHADEMA APATIKANA AKIWA HOI MBEYA


Kijana Mdude Nyagali, mfuasi wa Chadema amepatikana eneo la Inyala Mbeya Vijijini baada ya kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana Jumamosi jioni wiki iliyopita mjini Vwawa-Mbozi mkoani Songwe.

Akizungumza kwa simu jana usiku huu, mmoja wa watu waliokwenda kumbeba eneo la tukio, Anangisye Kwame amesema wameshamchukua na kuelekea naye Hospitali kwa ajili ya matibabu.

"Ndio, tupo nae kwenye gari, tunarudi mjini, anaongea vizuri. Ila tunaenda naye kwanza hospitali," amesema.

Awali, taarifa za kupatikana kwa Mdude, zilitolewa na Diwani wa Kata ya Nsalala, Mbalizi, Kisman Mwangomale akisema amepigiwa simu na watu wa eneo la Makwenje Kijiji cha Inyala Mbeya vijijini, wakiomba msaada wa haraka kwenda kumbeba.

Mwangomale amesema, "kweli yupo mikononi mwetu kwa sasa baada ya mimi kupigiwa simu na watu wa kule, ndiyo nikaona njia ya haraka ni kuandika kwenye magroup ya whatsapp."

Mdude alidaiwa kutekwa Jumamosi wiki iliyopita na watu wasiojulikana ambao walifika ofisini kwake wakiwa na magari mawili yenye rangi nyeupe kisha kumchukua kwa nguvu na kumuingiza kwenye moja ya magari yao na kuondoka naye na kwenda kusikojulikana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post