Masoko Mapya ya Madini Yaingiza Bilioni 34.3 Kwa Mwezi Mmoja

Na Frank Mvungi- MAELEZO
Dhahabu ya Bilioni 34.3 imeuzwa katika Kipindi cha mwezi mmoja kupitia katika masoko 21 yaliyoanzishwa kwa ajili ya kuuza madini katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
 
Akizungumza katika mahojiano maalum na idara ya habari MAELEZO, Bungeni Jijini Dodoma Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko amesema kuwa kuanzishwa kwa masoko hayo kumekuwa chachu ya kuongeza mchango wa sekta ya madini katika kukuza uchumi na pato la Taifa kwa ujumla.
 
“ Katika kipindi cha mwezi mmoja tu yaani Machi 17 mpaka Aprili 17 mwaka huu,jumla ya kilo 409.3 za dhahabu pekee zenye thamani ya shiilingi bilioni 34.3 imeuzwa kupitia katika maduka yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali” Alisisitiza Biteko.
 
“Katika kilo hizo,Mkoa wa Geita umeongoza kwa kufanya biashara ya jumla ya kilo 289,Kahama kilo 44,Mara kilo 13,lakini cha kufurahisha zaidi ni kwa Wilaya ya Chunya ambako jumla ya kilo 52 zimeuzwa katika soko hilo zikiwa nia siku chache toka kufunguliwa kwake ,”,aliongeza, mheshimiwa Biteko.
 
Aidha mheshimiwa Biteko, katika mahojiano hayo maalum,ameeleza kuridhishwa na biashara inayofanyika katika maduka hayo ya madini kote nchini na kueleza kuwa licha ya mafanikio hayo yaliyofikiwa katika kipindi kifupi,serikali inashughulikia changamoto ndogondogo ikiwemo wafanyakazi,mashine za XRF na idadi ya watoa vibali.
 
Akifafanua amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuona sekta hiyo inatoa mchango stahiki katika kujenga uchumi na kuchangia maendeleo hapa nchini ndio sababu mkazo umewekwa katika kusimamia sekta hii.
 
Pia aliwataka wachimbaji wadogo na madalali wa madini kuhakikisha kuwa wanatumia masoko hayo kikamilifu na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufutiwa leseni jambo alilosema serikali haipendi,
 
Akizungumzia mikakati ya kusimamia sekta hiyo Mhe. Biteko amesema kuwa ni pamoja na kushirikisha wachimbaji wadogo katika kuhakikisha kuwa vitendo vya utoroshaji wa madini unakomeshwa ili kulinda mapato ya Serikali.
 
Aliongeza kuwa hatua nyingine ni usimamizi wa karibu katika maeneo yote ya uzalishaji wa madini ya aina mbalimbali na kuchukua hatua za kutatua changamoto mbalimbali katika sekta hiyo.

Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Waziri Biteko amebainisha kuwa masoko mengine 7 yanatarajiwa kufunguliwa.
 
Baadhi ya Mikoa ambayo imeshafungua masoko ya kuuza madini ni pamoja na Geita, Dodoma, Mwanza, Tabora, Shinyanga, Morogoro, Mbeya, ambapo tayari mikoa 21 imeshafungua maduka hayo hadi sasa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli alilolitoa kwa wakuu wa mikoa wote hapa nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post