Video : DAKIKA 11 ZA MASELE AKIWASHA MOTO BUNGENI DHIDI YA TUHUMA ZA SPIKA NDUGAI

Spika Job Ndugai na Mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Stephen Masele.

Ukumbi wa Bunge jana ulikuwa wa moto. Hivi ndivyo unavyoweza kuelezea kile ambacho kilitokea bungeni wakati Spika Job Ndugai na Mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Stephen Masele kutuhumiana.

Masele ambaye ni Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP) alitumia dakika kumi na moja alizopewa na Spika Ndugai kuomba radhi, kutoa tuhuma mbalimbali dhidi ya kiongozi huyo wa Bunge baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumtia hatiani kwa makosa manne.

Masele, alisema barua ya Ndugai kwenda kwa Rais wa PAP, Roger Dang ingeweza kumng’oa huku akishangaa kwa nini hakutaka kumsikiliza kabla ya kuchukua hatua hiyo.

“Rais wa PAP aliitaka hii barua yako kutaka kunivua. Kwa kuzingatia barua yako Spika ninayekuheshimu, nilitafakari sana kwa maslahi ya wabunge, Taifa na kijana ninayekua katika uongozi. Nilifikiria haraka na busara yangu iliniongoza kama Spika ananisimamisha bila kunisikiliza, ndio sababu ya kukata rufaa na ndio sababu ya kuwasiliana na mwenyekiti wa CCM na mwenyekiti wa wabunge wa CCM bungeni ambaye ni Waziri Mkuu.”

Huku akishangiliwa na wabunge wa pande zote, Masele alianza kwa kumshukuru Mungu kisha kusema, “ninaomba kutumia fursa hii kukuomba radhi wewe (Spika) binafsi na familia yako kwa usumbufu wowote ulioupata kupitia sakata hili. Niwaombe radhi wabunge wenzangu kwa usumbufu mlioupata. Nitumie nafasi hii pia kuwaomba radhi viongozi wangu wakuu, mwenyekiti wa chama changu Rais John Magufuli, Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) ambaye ni mwenyekiti wetu wa wabunge wa CCM kwa usumbufu wowote walioupata kutokana na jambo hili,” alisema.

Alisema anaomba rekodi ibaki sawa kuwa, “makosa yaliyoorodheshwa katika shtaka langu, ningefurahi kama hansard ya kikao ingeletwa katika Bunge hili ili wabunge na Watanzania wajue ukweli.”

Alianza kwa kutoa barua ya mwaliko wa kuhudhuria kikao cha Bunge la PAP na kuionyesha akisema, “utaratibu wa Bunge, huwa hatuji kuomba kibali, bali tunatoa ‘notification’ kwa hiyo mheshimiwa Spika nilileta notification katika ofisi ya Katibu wa Bunge. Tuhuma zinasema nimesafiri bila kibali, sisi tuko wanne, kwa nini Masele ninaadhibiwa mimi na wabunge wenzangu wasichukuliwe hatua?”

Huku ukumbi wa Bunge ukiwa kimya kumsikiliza, Masele alisema barua ambayo Spika alimwandikia Mei 16, aliipata saa 11 jioni ikimtaka awe amefika Tanzania Jumanne ya Mei 17 saa 4:00 asubuhi jambo ambalo lingekuwa gumu kutokana na kubadili tiketi ya ndege na hakuwa na fedha za kulipia hoteli na Bunge kutowalipa posho za kujikimu.

Alisema barua hiyo ilitaka kutumiwa na Rais wa PAP ambaye ni raia wa Cameroon kumng’oa kwenye wadhifa huo wa Makamu wa Rais wa PAP na mjumbe wa Bunge hilo.

Alisema alifikiria haraka na busara yake ikamuongoza kukata rufaa na ndio sababu ya kuwasiliana na mwenyekiti wa CCM na Waziri Mkuu ambaye ni mwenyekiti wa wabunge wa CCM.

Akizungumza kwa kujiamini, Masele alisema, “Niliwaandikia ujumbe na kuwatumia barua hii nikiomba ushauri. Barua hii ilitaka kutumika kunichinja, kukata kichwa changu nisiwe Makamu wa Rais na mjumbe wa PAP, kama ni mbunge wa Bunge hili ungefanya nini.”

Alisema Spika kwa nafasi yake angeweza kumpigia simu na kumuuliza kipi kimetokea lakini aliamua kumhukumu bila hata kamati ya maadili kumsikiliza na “ninasikitika kwamba sikuchonganisha muhimili, nisingeweza kupeleka jambo hili kwa waziri au katibu wa wabunge wa CCM.”

Alisema video iliyoonekana, ilikuwa sehemu ya sekunde tu ikimwonyesha akisema kwamba anaungwa mkono na Serikali na barua ya Spika haitambui.

“Spika nimekubali mimi ni kijana, nimebeba dhamana, ninakuomba radhi. Ieleweke sikufanya kwa makusudi kukuvunjia heshima, kukudharau, nilipokea wito wako saa 11 jioni na kunitaka kesho yake nifike Dodoma saa nne asubuhi. Nimekwenda Afrika Kusini bila kupewa posho, nauli, tiketi na ningepata wapi watu wa kulipa bili hotelini?” alisema

Masele aliyewahi kuwa naibu waziri wa nishati na madini na Ofisi ya Makamu wa Rais katika utawala uliopita alisema, “na wakati huo Rais PAP alikuwa na hatia za udhalilishaji wa kijinsia, natambua Rais wa PAP anafanya mawasiliano na wewe (spika) ili mimi nisirudi PAP, najua na ninatambua.”

“Naamini umefanya ushauri wa kutosha, nimekubali makosa, kwa heshima ya Bunge langu, nakuja mbele yako kuomba radhi kwa usumbufu ulioupata, nashukuru kwa nafasi hii, Bunge na Watanzania kujua ukweli,” alisema.

Masele alimaliza kwa kusema amekuwa mbunge miaka tisa na hajawahi kuitwa katika kamati yoyote ya nidhamu, sijawahi kufanya kosa lolote, najitambua, najiheshimu huku akisema kwa kutumia kanuni ya 68(1) kanuni inayovunjwa ya 63(1) kwa mwenyekiti wa kamati kuleta taarifa yenye upungufu, alitoa hoja ya kukataa ripoti yake.

Chanzo - Mwananchi

                    SOMA ZAIDI <<HAPA>>

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post