MASELE : SIJAWAHI KUKURUPUKA

Mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM) Stephen Masele, amesema, hajawahi kukurupuka katika kusimamia jambo lolote. 

Alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kutoka kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge jijini Dodoma kuhusu tuhuma za utovu wa nidhamu. 

“Fuatilia rekodi zangu huko nyuma, chochote ninachokisema ninasimamia haki, ukweli na ninaheshimu viongozi wenzangu,” amesema Masele.

Masele amefika mbele ya kamati hiyo baada ya Job Ndugai, Spika wa Bunge kudai kwamba, mbunge huyo amekuwa akitoa maneno ya hovyo hovyo na hata kugonganisha mihimili miwili ya dola.

Masele ambaye ni Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), alifika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Emmanuel Mwakasaka, Jumatatu ya tarehe 20 Mei 2019 kama alivyoelekezwa na Spika Ndugai.

Mbele ya wanahabari Masele alisema, anatambua miiko ya uongozi kwa kuwa, ameshika nafasi mbalimbali ikiwa ni pamoja na unaibu waziri akisisitiza kuwa, hajawahi kukurupuka katika kufanya uamuzi ama kwenye misimamo yake.

“…ninasimamia haki, ukweli na ninaheshimu viongozi wenzangu , amesema Masele na kuongeza “nimekuwa naibu waziri, natambua miiko ya uongozi.

“Nawahakikishie Watanzania kwamba, kile nilichokuwa nasimamia ni misingi ya haki za binadamu na kufanya hivyo nisitafsiriwe kwamba, ni utovu wa nidhamu.”

Amesema kuwa, amelelewa kwenye familia yenye maadili mema na pia amepitia kwenye umoja wa viajana hivyo hana tabia ya kudharau viongozi wake

“Ninaheshimu sana viongozi wangu, nimelelewa vizuri na wazazi wangu, na chama change pia. Nimetokea umoja wa vijana kuanzia ngazi ya chini mpaka ngazi ya kitaifa na kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa,” amesema.

Masele hakueleza namna ya mjadala ulivyokuwa mbele ya Kamati ya Maadili, ila ameeleza kuwa na matumaini ya kutendewa haki.

Hata hivyo, Spika Nduga alisema kuwa, baada ya Masele kuhojiwa na kamati hiyo, atahojiwa pia na Kamati ya Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Chanzo- Mwanahalisionline

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post