Kikwete Alia na Changamoto Ya Utawala Bora Afrika

Rais  mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amesema kukosekana kwa umoja, utawala bora na uwepo wa umaskini ni miongoni mwa matatizo yanayozikandamiza nchi nyingi za Afrika, hivyo kuzikosesha maendeleo.

Akizungumza kwenye Tamasha la 11 la Kigoda cha Mwalimu Nyerere,Kikwete alisema licha ya kufanikiwa kupata uhuru, nchi nyingi za Afrika ni maskini.

Alisema wakati viongozi kadhaa wa Afrika walipata nafasi ya kukutana kwenye nchi za Ulaya waliunganisha nguvu zao za kiharati katika kutetea Afrika, hatimaye kufanikiwa kusaidia kupatikana kwa uhuru kuanzia mwaka 1950 hadi 1964.

Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi kwenye tamasha hilo lililokusanya wasomi wa viwango mbalimbali kutoka katika nchi tofauti, alisema kuna nchi bado zinatawaliwa kijeshi, viongozi wengine wamekaa madarakani kwa muda mrefu.

Alisema kuna wakati viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) walianzisha utaratibu wa kujitathmini ambapo viongozi waliitwa na kupewa maoni ya kujisahihisha, wapo waliofanyia kazi na wengine waliyaweka.

Akizungumzia kuhusu umasikni Kikwete alisema katika nchi 30 maskini duniani 27 ni kutoka Afrika.

“Watu wetu wanakabiliwa na umaskini mkubwa sana, haya ndiyo mambo ambayo Afrika inatakiwa iungane kukabiliana nayo, tumetoka mbali na tulikuwa na mafanikio kwenye kujipatia uhuru, lakini licha ya jitihada tumeshindwa kujikomboa kutoka kwenye hali duni,” alisema.

Alisema hali ya uanaharakati iliyoanzishwa na waasisi wa nchi za Afrika kabla na baada ya uhuru, walibaini kuwapo kwa matatizo hayo walikubaliana kuyatatua kwa umoja, lakini hadi sasa harakati hazijafanikiwa.

Kikwete alisema katika nchi 54 zilizopo katika bara la Afrika, ni nchi moja pekee ndiyo inatajwa kuwa imeendelea nayo ni Mauritius wakati 27 kati ya hizo zipo katika uchumi wa kati.

Alibainisha kuwa nchi zimekosa umoja hata katika kujitafutia masoko ya bidhaa mbalimbali, kila moja inajitafutia binafsi, hivyo elimu inahitajika ili kuwezesha waafrika kupambana kuunganisha nguvu zao katika kujitafutia maendeleo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post